MAJERUHI WAONGEZEKA YANGA

WAKATI  kipa namba moja Yanga, Yaw Berko bado majeruhi kiasi ch kushindwa kufanya mazoezi na wenzake, hali imezidi kuwa mbaya baada ya jana viungo watatu Nurdin Bakari, Rashid Gumbo pamoja na Godfrey Bony kuumia wakati wa mazoezi na kushindwa kuendelea kujumuika na wenzao.
Wingi wa majeruhi umezidi kuiandama klabu ya Yanga ambayo inakabiliwa na mchezo mgumu mwishoni mwa wiki dhidi ya Maafande wa JKT Ruvu baada ya kipa wao Yaw Berko kuendelea kukaa nje kutokana na kusumbuliwa na goti alipoumia kwenye mchezo wa kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar ingawa ameanza kufanya mazoezi kidogo.
Daktari msaidizi wa timu hiyo, Nassor Matuzya ambaye anakaimu nafasi ya daktari wa timu hiyo, Juma Sufiani anayeumwa hivi sasa alisema jana jana kuwa ni kweli wakati wa mazoezi ya juzi Nurdin aliumia mkono akiwa katika harakati za kuwania mpira huku Gumbo akiumia kifundo cha mguu pamoja na Bony.
Matuzya alisema wachezaji hao wanajumuika na mwenzao Berko ambaye bado na yeye anaendelea na matibabu kutokana na kuwa majeruhi hivyo timu hiyo kuongeza idadi ya majeruhi.
"Kwa kweli tunasikitika katika hili, lakini tuna amini watapona haraka na kurudi kuendelea kufanya mazoezi na wenzao, kama unavyofahamu Jumamosi tuna mchezo mwingine ambao utakuwa mgumu kati yetu na JKT Ruvu na wachezaji hawa uwezekano wa kucheza ni mdogo na utategemea na hali zao zitakavyokuwa,"alisema Matuzya.
Yanga inayojiandaa na mashindano ya klabu bingwa Afrika mwezi ujao itakutana na JKT Ruvu ikiwa ni mchezo wao wa pili wa mzunguko wa lala salama wa Ligi Kuu Tanzania bara baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya Moro united kutoka sare ya 2-2.

Comments