KIFA YAIPIGA JEKI VILLA SQUAD

CHAMA cha Soka cha Wilaya ya Kinondoni (KIFA) jana kilikabidhi viatu seti 11 kwa timu ya Villa Squad ambayo inashiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambayo leo inaingia katika mzunguko wa lala salama utakaotoa wawakilishi wa nchi katika mashindano ya kimataifa.
Akikabidhi msaada huo jana kwenye ofisi za KIFA, Makamu wa Kwanza wa KIFA, Tom Mazanda, alisema kuwa msaada huo wa viatu waluoukabidhi wanaamini utasaidia kuwafanya wachezaji wao waweze kufanya vizuri katika ligi hiyo wakiwa ni timu pekee kutoka katika wilaya ya Kinondoni.
Mazanda alisema kuwa viatu hivyo walivyokabidhi jana vina thamani ya Sh. milioni moja na hiyo si mara ya kwanza kwa uongozi wake kuisaidia timu hiyo.
"Tunawaomba mpokee msaada huu ili uweze kuwasadia na tunaahidi kuendelea kuwasaidia kwa kila hali, tunawatakiwa mafanikio katika mzunguko huu wa mwisho," alisema Mazanda.
Aliwataka pia wadau wengine kujitokeza kuisaidia Villa Squad ambayo bila ya misaada ya wadau wachezaji wake wanafanya maandalizi kwa matatizo.
Akipokea msaada huo, Kaimu Katibu Mkuu wa Villa Squad, Frank Mchaki, aliwashukuru viongozi wa KIFA na kusema kwamba timu hiyo ni ya wadau wote wa Kinondoni hivyo kila mwenye uwezo anatakiwa ajitokeze kuisaidia na hatimaye mafanikio yatapatikana.
Mchaki alisema kwamba mpira una gharama kubwa hivyo viongozi peke yake hawawezi kuiongoza Villa Squad bila ya ushirikiano kutoka kwa wanamichezo wote wa wilaya hiyo.
Villa Squad ilirejea katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu na leo itashuka dimbani kwenye uwanja wa Chamazi kuikaribisha Kagera Sugar kutoka mkoani Bukoba.

Comments