JKT RUVU, YANGA KUCHEZA SAA 12


Mechi namba 100 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya JKT Ruvu na Yanga itachezwa kesho (Januari 28 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo. Lakini mechi hiyo sasa itaanza saa 12 kamili jioni badala ya saa 10 kamili jioni.
Mabadiliko hayo ya muda yamefanyika ili kutoa nafasi kwa timu ya Taifa ya Namibia kufanya mazoezi kwenye uwanja huo saa 10 jioni kabla ya mechi yao ya Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Twiga Stars itakayochezwa Jumapili (Januari 29 mwaka huu) kwenye uwanja huo kuanzia saa 10 kamili jioni.
Kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya AWC yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), siku moja kabla timu ngeni ni lazima ipewe fursa ya kufanya mazoezi kwenye uwanja utakaotumika kwa mechi katika muda ule ule.
Pia kutokana na mechi ya Twiga Stars na Namibia, mechi namba 102 kati ya Moro United na Azam iliyokuwa ichezwe Januari 29 mwaka huu Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, sasa itachezwa Januari 30 mwaka huu kwenye uwanja huo huo.
Mabadiliko hayo hayajaathiri mechi nyingine za mzunguko wa 15. Mechi hizo ni kati ya Villa Squad na Toto African (Januari 28 mwaka huu- Uwanja wa Chamazi), Ruvu Shooting na Kagera Sugar (Januari 28 mwaka huu- Uwanja wa Mlandizi), Mtibwa Sugar na Coastal Union (Januari 29 mwaka huu- Uwanja wa Manungu), African Lyon na Polisi Dodoma (Februari 1 mwaka huu- Uwanja wa Chamazi) na Simba na JKT Oljoro (Februari 1 mwaka huu- Uwanja wa Taifa).
Viingilio kwa mechi za Uwanja wa Taifa ni sh. 3,000 viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 VIP C na B, na sh. 15,000 VIP A wakati Uwanja wa Chamazi ni sh. 3,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa jukwaa.

Comments