GIBSON ATUA EVERTON

Everton imekamilisha usajili wa Darron Gibson kutoka Manchester United kwa mkataba wa miaka minne na nusu kwa kiasi cha fedha ambacho hakijatajwa.
Gibson amehamia Everton na kuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na klabu hiyo katika dirisha dogo la usajili la mwezi Januari.
Gibson, 24, alisema: "Niko tayari na changamoto na nafikiri ilikuwa wakati mzuri kwangu kuhama kutoka Manchester United."
Kiungo huyo alifunga magoli 10 katika michezo 60 aliyochezea United. Gibson ametokea katika kikosi cha vijana cha United, na alizaliwa Ireland ya Kaskazini lakini aliamua kuichezea Jamhuri ya Ireland, na amechezea timu hiyo mara 17.
Jaribio la kutaka kuhamia Sunderland lilishindikana kutokana na kutokubaliana maslahi binafsi, lakini pia hakuwa akipata nafasi katika kikosi cha kwanza cha United.
Anakuwa mchezaji wa pili kuwasili Goodison Park mwezi huu baada ya Landon Donovan kusajiliwa kwa muda mfupi akitokea LA Galaxy.
Meneja David Moyes pia alikuwa na matumaini ya kusajili mshambuliaji, lakini atalazimika kutazama zaidi upande wa mabeki wa kati, hasa kutokana na kuumia goti kwa Phil Jagielka na Sylvain Distin kujeruhiwa katika mchezo dhidi ya Tottenham ambapo walifungwa 2-0.

Comments