Dempsey aiteketeza Newcastle kwa 'hat-trick'

Clint Dempsey alipata 'hat-trick', magoli matatu katika mechi moja, wakati alipoiwezesha Fulham kuizaba Newcastle magoli 5-2.
Clint Dempsey
Dempsey alipata magoli matatu katika mechi dhidi ya Newcastle
Fulham, ikichezea uwanja wa nyumbani wa Craven Cottage, ilikuwa imefungwa bao la kwanza na Danny Guthrie, kabla ya Danny Murphy kutumia nafasi ya mkwaju wa penalti kusawazisha na kuipatia Fulham fursa ya kuzinduka na kuanza kufunga magoli.
Kisha Dempsey alifunga bao lake la kwanza, na kufululiza wavuni la pili, kabla ya mwenzake Bobby Zamora kufunga lingine la mkwaju wa penalti, na ikawa ni 4-1.
Bao la Hatem Ben Arfa liliwapa matumaini Newcastle kwa muda mfupi, kabla ya Dempsey kufunga bao la tano na kuwavunja moyo kabisa.
Mabao mawili ya Robbie Keane, mchezaji wa Aston Villa, yaliwaangamiza Wolves, ambao wamo katika hatari ya kuondolewa katika ligi kuu ya Premier.
Darren Bent alipewa nafasi ya kupiga penalti baada ya kuchezewa vibaya, na pasipo kusita, aliiwezesha Villa kutangulia, kabla ya Michael Kightly kusawazisha.
Wolves walipata kwa muda nafasi ya kuongoza baada ya Roger Johnson kuusindikiza mpira wa kona, na David Edwards kufunga kwa kichwa, akimwacha kipa Shay Given akiduwaa.
Lakini hatimaye mkwaju wa Keane katika kipindi cha pili ukayafanya matokeo kuwa 2-2.
Karl Henry alionyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Marc Albrighton, na kufuatia tukio hilo, Keane akauelekeza mkwaju hadi wavuni kuandikisha bao la tatu, na Villa kushinda 3-2.
Katika mechi nyingine, Everton na Blackburn waliondoka na sare ya 1-1.
Tim Cahill alipata bao la kwanza, na la utata, kwa kufunga baada ya Maroune Fellaini kuuweka mpira sawasawa kwa kutumia mkono, jambo ambalo lilimpita mwamuzi.
Blackburn Rovers walisawazisha kupitia mchezaji David Goodwillie.
Chelsea waliendelea kusononeka, baada ya kutofungana na Norwich, na mshambulizi wa Chelsea, Fernando Torres, akicheza mchezo wake wa 17 pasipo kufunga goli.
Magali ya Heidar Helguson, Akos Buzsaky na Tommy Smith yaliinyanyua QPR kutoka hatari ya kushuka daraja, na sasa wakiiacha Wigan ikiendelea kukandamizwa katika nafasi ya mwisho ya ligi kuu ya Premier.
QPR iliishinda Wigan magoli 3-1.
Stoke nayo ilifungwa na West Brom magoli 2-1, huu ukiwa ni ushindi wa kwanza wa West Brom mwaka 2012.
Sunderland iliweza kuishinda Swansea magoli 2-0, na timu hiyo chini ya meneja mpya Martin O'Neill kukomesha mchezo laini wa Swansea, ambayo ilikuwa imecheza mechi nne mfululizo pasipo kushindwa.
Mchezo wa mwisho Jumamosi ulikuwa ni kati ya Bolton na Liverpool, na ambao ulikwisha kwa ushindi wa Bolton magoli 3-1.
Mechi inayozungumzwa sasa ni ya Jumapili, kati ya Arsenal na Manchester United.
Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ikishirikiana na redio washirika, itakutangazia moja kwa moja mechi hiyo.

Comments