BECKHAM ANABAKI MAREKANI, PSG WAISHIA KUNAWA

DOHA, Qatar KIUNGO David Beckham anajiandaa kuendelea kuichezea Los Angeles Galaxy baada ya kukataa kujiunga na Paris Saint-Germain, klabu hiyo ya Ufaransa ilisema jana.
Baada ya wiki za majadiliano na PSG, kiungo huyo mwene umri wa miaka 36 na Nahodha wa zamani wa England ameamua kutoiacha familia yake Marekani.
“David Beckham haji,”alisema rais wa PSG, Nasser al-Khelaifi akiwa katika michuano ya tenisi ya Qatar Open. “Tunajisikia vibaya sana. Lakini pande zote zimekubaliana itakuwa vizuri kuachana na mpango huo… labda baadaye.”
Mkataba wa awali wa miaka mitano wa Beckham na Galaxy ulimalizika alipouiwezesha klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Marekani MLS, Novemba, mwaka jana na tangu wakati huo amekuwa akitakiwa na klabu kadhaa Ulaya.
Beckham anaweza kuongeza mkataba mpya wa mwaka mmoja na Galaxy, ambayo inamlipa mshahara wa dola za KImarekani Milioni  6.5 kwa mwaka.
Vyombo vya habari viliripoti kuwa atakuliwa mara mbili ya fedha hizo akitua PSG, ambayo wamiliki wake kutoka Qatar wametumia zaidi ya dola za Kimarekani Milioni 100 kununua wachezaji katika kipindi cha miezi sita tangu waichukue.
Beckham na mkewe Victoria, mwimbaji wa zamani wa kundi la Spice Girls, walihamia California mwaka 2007 baada ya mkongwe huyo kuondoka Real Madrid.
Wawili hao kwa sasa wana watoto wanne na walifikia uamuzi wakati wa Krisimasi walipokuwa mapumzikoni Ulaya kwamba hawatarejea Ulaya moja kwa moja.
Mafanikio ya karibuni ya Galaxy na kumsajili Nahodha wa Ireland, Robbie Keane inaonekana kumvutia Beckham kwamba klabu hiyo ya LA inaweza kumfanya atomize malengo yake katika siku za mwisho za maisha ya soka yaliyoanzia Manchester United.
Beckham ameelezea matumaini yake ya kukichezea kikosi cha England katika Michezo ya Olimpiki mwaka huu London. Msimu mpya wa MLS utaanzaa Machi.

Comments