YANGA WAJITOA KOMBE LA MAPINDUZI

UONGOZI wa Yanga umesema hautashiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa vile hakuna barua ya mualiko rasmi iliyofika kwao.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi imepangwa kufanyika Zanzibar kuanzia Desemba 31.
Siku hiyo mechi ya ufunguzi itakuwa ni kati ya timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes na ile ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kabla michuano hiyo haijaanza rasmi Januari 2.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Yanga, Celestine Mwesigwa alisema hawawezi kushiriki michuano hiyo kwani mpaka sasa wanasikia ushiriki wao kwenye vyombo vya habari tu badala ya wahusika
kuwapelekea barua rasmi.
“Sijui kwa wenzetu, lakini mpaka sasa sisi kama Yanga hatujapata barua rasmi kutoka kwa hao waandaaji tunasikia tu tukitajwa kwenye vyombo vya habari kwamba tunashiriki,” alisema.
Mbali na Yanga, timu nyingine kutoka Bara zinazotangazwa kushiriki michuano hiyo ni Azam na Simba.
Kwa upande wa Zanzibar, timu zitakazoshiriki ni KMKM, Miembeni, Kikwajuni, Mafunzo na Jamhuri.
Alipoulizwa msemaji wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Munir Zakaria juu ya hilo alisema chama chake hakihusiki katika hilo kwani si waandaaji.
“ZFA haiandai mashindano hayo hivyo hatuhusiki na lolote kuhusu ushiriki wa timu, kuna kamati inashughulika na hilo labda mtafuteni Farouk Karim ndio msemaji wao,” alisema.
Juhudi za kumpata Farouk hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi hakujibu.

Comments