YANGA KUIKUSANYIA NGUVU ZAMELEK HAPA HAPA

MABINGWA wa soka nchini, Yanga ya jijini Dar es Salaam, sasa italazimika kufanya maandalizi yote ya kuwavaa Zamalek ya Misri wakiwa nyumbani baada ya ndoto zao kupiga kambi nje ya nchi kufutwa na ukata unaoikabili timu hiyo.
Yanga itashuka dimbani kupambana na Zamalek katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Soka Afrika baadaye mwakani.
Awali mabingwa hao walipanga kuweka kambi Afrika Kusini na Msumbiji kujiandaa na mechi hiyo kabla ya kucheza mchezo wake wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia hali hiyo kocha wa Yanga, Kostadin Papic alisema jana kuwa wameamua kufuta mipango yao ya kuweka kambi nje ya nchi kutokana na gharama kubwa za kupeleka timu huko.
Alisema kutokana na gharama hizo wameona ni bora maandalizi yao yakayafanyia hapa na kuzileta timu nchini badala ya kwenda nje ya nchi.
“Kama fedha zingetosha kufanya na maandalizi nje ya nchi, tungeweza kuweka kambi huko, lakini hali imekuwa kinyume kwani fedha ni nyingi na hakuna jinsi zaidi ya kuziita timu kuja hapa nyumbani na kucheza nao," alisema.
Alisema kuwa mipango imeanza kuzialika timu za Uganda, Kenya, Zambia na Malawi ili kuja kujipima nchini.
“Siwezi kusema ni timu zipi zitakuja, lakini tuna mipango thabiti ya kuhakikisha tunacheza mechi nyingi za kujipima nguvu hapa nyumbani na si vinginevyo,” alisema Papic.
Tayari Yanga imepanga kucheza na mabingwa wa Malawi, timu ya shirika la Umeme la Escom United Jumamosi ya Desemba 24 kwenye Uwanja wa Taifa jijini.
Aidha kuna mipango ya kucheza na timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwa moja ya jaribio kubwa kabisa kabla ya kupambana na Zamalek. Mipango ya mechi dhidi ya TP Mazembe ipo katika hatua za awali.

Comments