WENGER AFUNGA MDOMO SUALA LA HENRY KUREJEA EMIRATES

Arsene Wenger amekataa kuzungumza lolote kuhusiana na uvumi uliozagaa kwamba Thierry Henry huenda akarejea tena katika klabu ya Arsenal.
Wenger asema hakuna kinachoendelea kumsajili Henry
Wenger asema hakuna kinachoendelea kumsajili Henry

Henry, mwenye umri wa miaka 34, ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika klabu ya Arsenal enzi za uchezaji wake na ambaye hivi karibuni sanamu yake ilizinduliwa nje ya uwanja wa Emirates kwa heshima yake, haitajiki kurejea katika klabu yake ya New York Red Bulls hadi mwezi wa Machi.
Lakini Wenger alisema: "Hakuna stori na kama tutamsajili yeyote tutawaarifu.
"Nina miaka 15 nchini England. Kamwe sijawahi kutamka kuhusu usajili wa mchezaji yeyote kabla ya kukamilisha usajili."
Wiki iliyopita, Wenger alisema "hakuna nafasi yoyote" ya kumsajili mlinzi wa Bolton Gary Cahill.
Lakini wakati huu Arsenal ikiwa inajiandaa kuwakosa washambuliaji wake wawili Gervinho na Marouane Chamakh mwezi wa Januari watakapokuwa katika mashindano ya Mataifa ya Afrika wakiwakilisha nchi zao, Wenger huenda anahisi Robin van Persie atakuwa anahitaji msaada.
Kabla ya sikukuu ya Krismasi, kulikuwa na fununu kwamba klabu hiyo ya kaskazini mwa London ilikuwa inafikiria kuiomba klabu ya Red Bulls kama wanaweza kumsajili Henry kwa mkopo wa miezi miwili hadi msimu wa Ligi ya Marekani utakapoanza.
Henry amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha Arsenal ili kujiweka sawa.
Lakini Wenger amesema: "Hakuna kilichofanyika tangu wiki iliyopita. Sitarajii chochote kwa wakati huu."
Walipocheza na Wolves, Arsenal wangeweza kumaliza kazi kama alivyokuwa akifanya Henry enzi zake alipoichezea klabu hiyo kwa miaka minane, ambapo alifanikiwa kupachika wavuni mabao 226 katika michezo 370 kabla ya kuhamia Barcelona.
Baada ya kuongoza kwa bao moja lililofungwa na Gervinho mapema kipindi cha kwanza, Wolves walisawazisha zikiwa zimesalia dakika chache kabla kumalizika kipindi cha kwanza wakati Steven Fletcher alipounganisha kwa kichwa mkwaju wa Stephen Hunt na mpira huo ukamshinda mlinda mlango wa Arsenal Wojciech Szczesny.
Lakini mlinda mlango wa Wolves Wayne Hennessey alifanya kazi kubwa kuinyima the Gunners pointi tatu ambazo zingeiinua timu hiyo hadi nafasi ya nne.
Sare ya 1-1 ilimhuzunisha sana Wenger, hasa kwa vile Wolves walilazimika kucheza wakiwa 10 kwa dakika 20 za mwisho baada ya kiungo wao Nenad Milijas kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea rafu mbaya Mikel Arteta.
"Tulijitahidi sana," Alisema Wenger. Tumepoteze nafasi nzuri na muhimu lakini hatuna budi kuangalia mbele, iwapo umecheza mechi 20, umeshinda 19, basi haikuwa siku yetu.
"Inaudhi, lakini nimeudhika zaidi na matokeo na si kwa kiwango cha kandanda tuliyocheza na moyo uliooneshwa na wachezaji.
"Mlinda mlango wao alicheza kufa na kupona. Wolves walipigana kiume na nawapongeza."

Comments