WATOVU WA NIDHAMU HAWANA NAFASI SIMBA 2012


UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umesema kuanzia mwaka 2012 hautawavumilia watovu wa nidhamu.Hatua hiyo inafuatia wachezaji wengi wa klabu hiyo kuendesha vitendo vya utovu wa nidhamu ndani na nje ya timu hiyo hali ilipelekea kuwafedhehesha viongozi na wanachama wa klabu hiyo kwa ujumla.Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alisema jana kwamba, uongozi na wanasimba wamechoshwa na wachezaji hao hivyo hautokuwa tayari kuwalea kundini katika mwaka ujao.Alisema kuwa uongozi hautamvumilia mchezaji yoyote ambaye ataonyesha utovu wa nidhamu hata kama ana kiwango cha hali ya juu katika kikosi chao watamuadhibu kwa mujibu wa sheria na kanuni za Shirikisho la soka barani Afrika (CAF).“Napenda kutoa salamu zangu za mwaka mpya kwa wachezaji wote wa Simba na kuwaambia kwamba, uongozi hautamvumilia mchezaji yoyote ambaye atatenda utovu wa nidhamu, tutamuadhibu kwa mujibu wa sheria za CAF,”Alisema.Aidha, Rage aliwapongeza wanachama wa klabu hiyo kwa kuwa watulivu kwa mwaka wote wa 2011 sambamba na kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu na viongozi pamoja na wachezaji wa timu hiyo.
 

Comments