UTEUZI WA KAMATI YA KUKAMILISHA MCHAKATO WA KUPATA VAZI LA TAIFA

WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO

TAARIFA YA VYOMBO VYA HABARI

Itakumbukwa kuwa Serikali, kupitia Idara ya Maendeleo ya Utamaduni ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, ilianzisha mchakato wa kupata Vazi la Taifa mwaka 2004.
 
Madhumuni ya kuwa na Vazi la Taifa ni kuongeza vitambulisho vya utaifa wa Watanzania.
 
Pamoja na vitambulisho vya utaifa wetu vilivyopo sasa, ambavyo hujumuisha mathalani Ngao ya Taifa, Bendera, ya Taifa, Wimbo wa Taifa, Lugha ya Taifa – Kiswahili, Mlima Kilimanjaro, Twiga, Mwenge wa Uhuru na kadhalika, ilionekana ni vema pia tukawa na vazi rasmi kwa wanaume na wanawake ambalo litaongeza utambulisho wa Taifa letu, kama ilivyo kwa mataifa mengine kama vile Swaziland, Ghana, Nigeria, Sudan, Ethiopia, Mali na kadhalika.

Mchakato wa kupata vazi hilo la Taifa, hadi sasa umeshapiga hatua kubwa. Wabunifu wazalendo wa mitindo ya mavazi wameshashirikishwa na kutoa mapendekezo yao.

Aidha, utafiti wa namna mataifa mengine yalivyoteua mavazi yao ya kitaifa umeshafanywa.
Hatua inayofuatia sasa ni ya kuwashirikisha wananchi kuhusu mapendekezo yaliyopo na hatimaye kupendekeza vazi mahususi linalotambulisha utaifa wa Watanzania.

Ili kuihitimisha kwa ufanisi kazi hii ya kupendekeza Vazi la Taifa, nimeteua Kamati maalum ya kukamilisha mchakato wa kupendekeza Vazi la Taifa. Wajumbe wa Kamati hiyo ni:-

1. Bw.Joseph Kusaga - Mwenyekiti
2. Bibi.Angela Ngowi - Katibu
3. Bw.Habibu Gunze - Mjumbe
4. Bibi.Joyce Mhaville - Mjumbe
5. Bw.Mustafa Hassanali - Mjumbe
6. Bw.Absaloom Kibanda - Mjumbe
7. Bw.Makwaiya Kuhenga - Mjumbe
8. Bw.Ndesambuka Merinyo - Mjumbe

Kamati hii itaanza kazi rasmi tarehe 15/12/2011 na itatakiwa kumaliza kazi hii tarehe 27/2/2012. Kamati itakabidhi taarifa yake kwangu tarehe 28/2/2012 saa 5 asubuhi katika ofisi ya Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo.

Dkt. Emmanuel John Nchimbi (Mb)
WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
Tarehe 12 Desemba, 2011

Comments