USAJILI WA GHAFLA KILI STARS WAZUA UTATA

USAJILI wa ghafla uliofanywa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), katika timu ya taifa ya Tanzania Bara, ‘Kili Stars’ inayoshiriki michuano ya CECAFA Challenge Cup juzi ulizua utata miongoni mwa mashabiki, wapenzi na wadau mbalimbali wa soka.

Kili Stars, juzi wakati ikicheza na Djibouti kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, katika orodha ya wachezaji ambayo ilikuwa imesainiwa na maofisa wahusika wakiwamo wasimamizi wa timu zote mbili, ilimuorodhesha mchezaji mwenye jezi namba 14, kama Rashid Yussuf, wakati hakuwa yeye, jambo ambalo lilizua utata na usumbufu pale alipoingia kipindi cha pili na kufunga bao la tatu.

Kutokana na orodha hiyo, mashabiki na wapenzi waliokuwapo uwanjani walitangaziwa na MC, mfungaji ni Yussuf Rashid, jambo lililojitokeza hadi kwa vyombo mbalimbali vya habari (si Tanzania Daima), vilivyoripoti mechi hiyo, wakati ukweli mfungaji alikuwa Hussein Javu, anayekipiga klabu ya Mtibwa Sugar, ambaye katika usajili wa awali uliowasilishwa CECAFA alikuwa ametemwa sambamba na nyota wengine akiwamo Gaudance Mwaikimba, mlinda mlango Deo Mushi na wengineo.

Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, alisema ni kweli Javu hakuwemo katika usajili wa awali, lakini walimuongeza juzi na sheria zinaruhusu kumuondoa mchezaji ambaye bado hajatumika na kusajili mwingine.

Wambura alisema ni kosa lililofanyika kumuorodhesha Rashid anayekipiga klabu ya Coastal Union ya Tanga katika mechi ya juzi, kwani tayari walikwisha muondoa na nafasi yake kuzibwa na Javu.

Comments