STARS KUJIPIMA UBAVU NA CONGO DRC


Timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imeomba kucheza mechi moja ya kirafiki na timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars). Mechi hiyo itafanyika Februari 23 mwakani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
DRC inatarajia kuwasili nchini Februari 18 mwaka huu ambapo itaweka kambi yake ya mazoezi hadi Februari 25 mwaka huu kujiandaa kwa mechi yao ya mchujo ya Kombe la Afrika (CAN) dhidi ya Mauritius.
Mechi ya DRC na Mauritius itachezwa Februari 29 mwakani nchini Mauritius. Stars yenyewe itacheza mechi ya kwanza ya mchujo kwa ajili ya fainali hizo za 2012 zitakazofanyika Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji. Mechi hiyo itachezwa Februari 29 mwakani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MCHUKA, NGAHYOMA
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya waandishi wa habari Halima Mchuka wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na John Ngahyoma wa Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC) vilivyotokea Desemba 29 na 30 mwaka huu.
Misiba hiyo ni mikubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Ngahyoma na Mchuka walishafanya kazi na TFF, hivyo mchango wao katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima. Ngahyoma baada ya kumaliza chuo cha uandishi wa habari mwishoni mwa miaka ya 80 alijiunga na Daily News ambapo alianza kwa kuripoti habari za michezo, hasa mpira wa miguu.
Mchuka naye tutamkumbuka kama mtangazaji wa mpira wa miguu ambapo mara ya mwisho tulifanya naye kazi kwa karibu mwaka 2005 ambapo alikuwa mjumbe wa Kamati ya Habari ya TFF kwa ajili ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati iliyofanyika jijini Mwanza.
TFF inatoa pole kwa familia za marehemu Ngahyoma, Mchuka, BBC na TBC na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha misiba hiyo mizito.
Mungu aziweke roho za marehemu Ngahyoma na Mchuka mahali pema peponi. Amina
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Comments