KLABU ya soka ya Simba
itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika pambano
litakalofanyika katika Uwanja wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam Jumamosi ya kesho.
Pambano hilo litakuwa la mwisho kwa Simba kucheza jijini Dar es Salaam
mwaka huu. Pambano hilo pia litakuwa la mwisho kwa Simba kabla haijakwenda
Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyopangwa kuanza Januari 2
mwakani.
Simba itaondoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar Januari Mosi mwaka huu (Jumapili).
Pambano dhidi ya Mtibwa litakuwa sehemu ya maandalizi ya michuano ya
Mapinduzi, Ligi Kuu ya Tanzania na michuano ya kimataifa ambayo Simba
itashiriki mwakani.
Mechi hiyo itakuwa ya kwanza
kwa Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovic, kukaa kwenye benchi la
ufundi na kuiongoza klabu yake hiyo ambayo ni mabingwa watetezi wa Kombe la
Mapinduzi na mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki
na Kati.
Viingilio katika pambano hilo vitakuwa ni Sh 5,000
kwa VIP na 2,000 kwa majukwaa mengine. Simba imeweka kiingilio hicho ili
kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuhudhuria pambano hilo na kusherehekea kumaliza mwaka salama
huku wakiitazama soka la uhakika.
Profesa Cirkovic ameahidi
kwamba kwenye pambano hilo
atashusha kikosi kamili cha wachezaji wa Simba ili kubaini ni kwa namna gani
wachezaji wake wameyaelewa mafunzo yake.
“Nawakaribisha wapenzi na
wanachama wa Simba na wapenda soka kwa ujumla waje kwa wingi kuiona Simba
ikicheza. Nimesikia kwamba uwanja wa Azam ni mzuri na utaendana na aina ya
mchezo ambao Simba itakuwa ikiucheza chini yangu. Nataka kuonyesha soka la
asili la Simba,” alisema.
Comments
Post a Comment