RAIS MSTAAFU ALI HASSAN MWINYI KUZINDUA 'MR. PRESIDENT' J'MOSI

RAIS Mstaaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa filamu ya ‘Mr President’ utakaofanyika kwenye hoteli ya Serena/Movenpick.
Meneja masoko wa kampuni ya Papazii Entertainment, ambayo inasimamia filamu hiyo, Vivian Sirikwa alisema pamoja na Mwinyi, wageni mbalimbali wamealikwa.
Alisema kuwa filamu hiyo ambayo kinara wake ni msanii maarufu nchini Steve Nyerere,inazungumzia maisha ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, kuanzia alipotoka na mpaka alipo sasa.
Aliongeza kuwa hata mazingira yaliyotumika katika kurekodi filamu hiyo ni yale ambayo Kikwete ameyapitia yaani katika mji wa Bagamoyo alipozaliwa, Dodoma na hata Ikulu.
“Hii ni zaidi ya filamu kwani washiriki wameweza kuuvaa uhusika kama ilivyokusudiwa, ninawaomba mashabiki na wadau wa tasnia nzima kuungana nasi katika hili kwanza kujitokeza katika uzinduzi, pia kuinunua pindi itakapoingia sokoni,”Alisema.
Baadhi ya wasanii walioshiriki mbali na Steve ambaye ameigiza kama Rais Kikwete ni pamoja na Jacquiline Wolper aliyeigiza kama marehemu Amina Chifupa, Juma Chikoka (Sugu), Rachel Haule (Halima Mdee), Aunt Harieth (Spika Anna Makinda), Maya (Salama Kikwete) na wengineo.
Aidha, baadhi ya fedha zitakazopatikana katika mnada utakaofanyika siku ya uzinduzi zitatumika kununulia vifaa ambayo vitapelekwa katika wodi ya watoto waliolazwa kwenye hospitali ya Mwananyamala.
Naye mtayarishaji na kinara wa filamu hiyo, Nyerere alisema kuwa fiamu hiyo ambayo imegharimu kiasi cha shilingi milioni 25, itakuwa sehemu moja tu na itauzwa kwa shilingi 5,000 kwa nakala.

Comments