RAIS JAKAYA KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA MR.EBBO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumamosi, Desemba 3, 2011, ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya mwanamuziki Abel Loshilaa Motika, maarufu kwa jina la usanii la Mr. Ebbo, ambaye alifariki dunia jana kwenye Hospitali ya Misheni ya Usa River, mkoani Arusha.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete ameeleza kuwa amepokea kwa mshituko na huzuni habari za kifo cha Bwana Motika ambaye Mheshimiwa Rais amemwelezea kama kijana ambaye ametoa mchango mkubwa katika fani ya usanii wa muziki katika kipindi kifupi cha maisha yake na kuwa atakumbukwa kwa mchango wake huo.
“Nimepokea kwa mshituko na huzuni habari za kifo cha Mr. Ebbo. Alikuwa kijana ambaye ametoa mchango mkubwa katika fani ya usanii wa muziki katika kipindi kifupi cha maisha yake. Hakuna shaka kuwa atakumbukwa kwa mchango huo,” amesema Mheshimiwa Rais na kuongeza:
“Nawatumieni wanafamilia, ndugu, jamaa, marafiki, wasanii na wapenzi wa muziki salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kutokana na msiba huu mkubwa. Napenda kuwajulisheni kuwa niko nanyi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo kwa sababu msiba wenu ni msiba wangu pia.”
“Naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema ambaye kwa mapenzi yake ameamua kumchukua mapema Bwana Ebbo, aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amen.”

Comments

  1. tulikupenda sana hasa kwa kazi zako na mfumo mzima wa maisha yako kwani ulikuwa tofauti na mtazamo wa wengi kwamba msanii ni lazima awe tofauti na jamii inayomzunguka lakini kwako ilikuwa ni tofauti.R.I.P kaka

    ReplyDelete

Post a Comment