PAPIC 'AFUNGUKA' YANGA, ATISHIA KUTIMKA IWAPO...

KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, Kostadian Papic ametishia kuachia ngazi iwapo uongozi wa klabu hiyo hautarekebisha baadhi ya mambo ambayo amesema hayaendi vizuri na kusema kuwa asilaumiwe kwa matokeo yoyote mabaya itakayoipata Yanga katika michezo yake ya hivi karibuni.
Papic ameamua kuanika ubabaishaji unaendelea ndani ya klabu hiyo ikiwemo kutokuwemo kwa ushirikiano wa kutosha toka kwa viongozi.
Alisema kuwa tangu aanze kuwanoa wachezaji wake mara baada ya kumalizika kwa likizo fupi, uongozi umeshindwa kutoa ushirikiano ikiwemo wa kutafuta sehemu maalum kwa ajili ya wachezaji wake kwenda kufanya mazoezi ya kujenga mwili 'gym'.
"NInafanya kazi katika mazingira magumu, viongozi hawanipi ushirikiano piundi ninapowatafuta kwa ajili ya kutaka kujua mustakanali mzima wa maandalizi ya timu...eti wanadai hakuna fedha, sasa tutafanyaje vizuri bila ya kujiandaa?Alihoji Papic.
Yanga ambayo inajiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania bara pamoja na mchezo wao wa ligi ya klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek  mwezi Februari mwakani, wachezaji wake pia wanahali ngumu kwani  hawapati fedha zao pamoja na kushindwa kupata chakula cha uhakika.
Papic aliongeza kuwa ukata huo umesababisha timu  kushindwa kufanya mazoezi kwa siku saba kwa kuwa wanakosa fedha za kukodi uwanja wa kufanyia mazoezi.
"Kwa hali hii ya ukata..siwezi kuahidi kwa mashabiki matokeo mazuri katika mechi zetu..., wachezaji hawana morari ya mazoezi kwa kukosa fedha na chakula kwa kweli hii hali inasikitisha kwa sababu hata kuingia Gym inashindikana kwa kukosa fedha," alisema Papic.
"Mashabiki wasije wakawalaumu wachezaji  au Kocha watakapoona timu inafanya vibaya.. hiyo ndio hali halisi klabuni," aliongezea kusema Papic.
Papic alisema kuwa kwa hali ilivyofikia anashindwa kuwalazimisha wachezaji kufanya mazoezi kwa kuwa anafahamu hali ngumu wanayokutana nayo.

Comments