NGASSA KUTOLEWA BURE MAREAKANI

UONGOZI wa Azam FC umesema utakuwa tayari kumtoa bure kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Mrisho Ngassa (pichani), kwa klabu ya Seattle Sounders ya Marekani.
Katibu Mkuu wa Azam FC, Idrisa Nassor, alilithibitishia Championi Jumatano kuwa, wao wako tayari kumtoa nyota huyo hata kama ni bure, lengo likiwa ni kumpa nafasi ya kuitangaza nchi katika soka la kimataifa.
Alisema kuwa muda wowote kuanzia sasa, uongozi wa Seattle Sounders utatua nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya mwisho kuhusiana na uhamisho wa Ngassa.
“Kuhusu kiasi cha fedha za uhamisho wake, sisi hatuangalii hilo sana, bali tunalenga kumsaidia Ngassa aende Marekani hata kama ni bure, licha ya ukweli kwamba soka linaendeshwa kwa gharama kubwa.
“Sisi hatuzingatii fedha ila uzalendo na mafanikio ya mchezaji husika ni masuala ya kipaumbele kwetu.
“Kutokana na hali hiyo, wakati wowote kuanzia sasa uongozi wa Seattle Sounders utawasili nchini ili kumalizia mazungumzo ya uhamisho wa mchezaji huyo. Februari mwakani anatakiwa ajiunge na klabu hiyo,” alisema Nassor.
Ngassa alifanya majaribio na Seattle Sounders Julai 20, mwaka huu katika mchezo kati ya timu hiyo dhidi ya Manchester United ya England ambapo Wamarekani hao walilala kwa mabao 7-1, huku Mtanzania huyo akiingia katika dakika ya 73 na kuonyesha kiwango.
NA GAZETI LA CHAMPION

Comments