MECHI KILI STARS, ZANZIBAR HEROES YAFUTWA



MECHI ya kirafiki baina ya timu ya soka ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ dhidi ya timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ iliyokuwa ifanyike Januari Mosi, 2012 katika uwanja wa  Amaan, Visiwani Zanzibar, imefutwa.
Mechi hiyo ni ambayo ilikuwa maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayotarajiwa Januari 2 na ikishirikisha timu kutoka Tanzania Bara na Visiwani humo.
 Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura amesema  kuwa hatua hiyo inafuatia Kilimanjaro Stars kutoweza kushiriki katika mchezo huo kutoweza kujiandaa na  wachezaji wengi wa timu hiyo na hasa wanaotoka katika klabu kubwa zikiwemo Azam, Yanga na Simba kwa sasa kuwa katika maandalizi ya kitimu kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu pamoja na mechi nyingine za kirafiki.
Wambura aliongeza kuwa, hata makocha wake Charles Boniface Mkwasa na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kwa sasa wanamajukumu mengine ya kuzinoa timu za Taifa.
“Kama mnavyofahamu makocha wa Kili Stars kwa sasa wote wana majukumu, Mkwasa anaendelea kukinoa kikosi cha Twiga Stars kinachojiandaa na mechi yake dhidi ya Namibia na Julio yupo Afrika Kusini na kikosi cha Vijana cha Dream Team ya Coca Cola”, Alisema.
Wambura aliongeza kuwa, wameshatuma barua pepe kwa Chama cha soka Visiwani Zanzibar kuwajulisha juu ya jambo hilo.

Comments