MASKAUTI NA MIAKA 50 YA UHURU WA TANGANYIKA

RAIS MSTAAFU ALI HASSAN MWINYI KUFUNGUA MASHINDANO YA SKAUTI PAMOJA NA MKUTANO WA MAKAMISHNA WA SKAUTI KWA NCHI ZA AFRIKA MASHARIKI NA KATI UNAO FANYIKA BAGAMOYO TAREHE 12 DESEMBA 2011.

Na: Hidan Ricco.
Katika kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania. Chama cha Skauti Tanzania kimepewa heshima ya kuwa wenyeji wa kuandaa mashindano ya skauti kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati, pamoja na Mkutano wa Makamishna wa skauti kutoka katika nchi za Afrika Mashariki na Kati. Mkutano pamoja na mashindano hayo tayari yameshaanza na yanaendelea huko Bagamoyo Mkoa wa Pwani kuanzia tarehe 9 hadi 13 Desemba 2011.
Akizungumza na vyombo vya habari, Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti Tanzania bw. Lawrence Mhomwa alitaja washiriki wa mashindano hayo kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, na wenyeji Tanzania.
Kila nchi imeleta vijana skauti 40 pamoja na Viongozi, Makamishna 6 kutoka katika nchi hizo.
Mjumbe muhimu katika mkutano huo ni Kamishna Mkuu wa Chama cha Skauti cha Kenya ni Mheshimiwa Kalonzo Musyoka ambaye pia ni Makamu Rais wa nchi hiyo tayari yupo nchini kuhudhuria sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania pamoja na kushiriki katika Mkutano huo.
Mkutano wa Makamishna wa Skauti unafanyika katika Hotel ya Kiromo iliyopo Wilayani Bagamoyo.
Rais Mstaafu Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi ambaye pia ni mmoja wa Wadhamini wa Chama Cha Skauti Tanzania, atafungua rasmi Mkutano huo pamoja na kutembelea kambi ya mashindano ya maskauti ambayo inafanyika eneo la Kaole Mamba Ranchi huko Bagamoyo.
Rais Mstaafu Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi atakutana na kuzungumza na Makamishna hao siku Jumatatu tarehe 12 Desemba saa 5 asubuhi na baadae kutembelea kambi ya mashindano ya skauti.
Mkutano wa Makamishna pamoja na mashindano ya skauti yatafungwa rasmi siku ya Jumanne tarehe 13 Desemba 2011, ambapo washindi wa mashindano hayo watazawadiwa zawadi mbalimbali za kiskauti ambazo zimeandaliwa na Sekretariat inayoratibu mashindano hayo.
Wazazi, ndugu na marafiki wa uskauti wanakaribishwa kuhudhuria sherehe hiyo.

HIDAN RICCO.
KAMISHNA MKUU MSAIDIZI
MAWASILIANO NA HABARI
CHAMA CHA SKAUTI TANZANIA
0715 – 0755 019288

Comments