MAN CITY YAIPIGA 'DENDA' ARSENAL

Manchester City siku ya Jumapili walithibitisha tena nia yao ya kuwa mabingwa wa ligi kuu ya Premier ya England msimu huu, kwa kuwafunga Arsenal goli 1-0.
Bao lake laiwezesha Man City kuendelea kuwa kileleni katika ligi kuu ya Premier
Kufuatia majirani Man United awali kuifunga QPR magoli 2-0, Man City ilifahamu lazima iwike katika uwanja wa nyumbani, na haikupoteza nafasi hiyo, wakati katika dakika ya 53, David Silva alipata bao la kwanza.
Awali, mkwaju mkali wa Mario Balotelli haukuweza kufua dafu, licha ya kuuelekeza vyema mpira wavuni.
Sergio Aguero alikuwa na nafasi ya kuongeza idadi ya mabao, lakini mpira wake ulipaa juu mno, huku Pablo Zabaleta naye akigonga mwamba.
Lakini Arsenal hawawezi kulalamika kwamba hawakupata nafasi ya kufunga mabao, kwani kipa Joe Hart aliweza kuiokoa timu yake kutokana na mikwaju ya Gervinho, Theo Walcott na Aaron Ramsey.
Hata mchezaji wa Arsenal Robin van Persie, ambaye amesifiwa sana kuichezea Arsenal vizuri mno hivi majuzi, alishindwa kupata bao lake la 20 msimu huu.
Baada ya kushindwa na Chelsea Jumatatu iliyopita, bila shaka Roberto Mancini amewathibitisha mashabiki kwamba Man City bado ina uwezo wa kupambana na timu yoyote ile, kama alivyokuwa amesema kabla ya mechi.
Kufikia sasa Man City inadumisha rekodi ya kutoshindwa katika uwanja wa nyumbani wa Etihad msimu huu, kwa asilimia 100.
Kati ya mechi 28 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, Man City imeondoka na sare katika mechi mbili tu.
Katika viwanja vingine, Aston Villa ilishindwa magoli 2-0 ilipocheza na Liverpool.
Tottenham nayo inashikilia nafasi ya tatu katika ligi ya Premier, baada ya kuifunga Sunderland bao 1-0.

Comments