HAPA SIMBA PALE KOTOKO NI FULL MZIKI KESHO UWANJA WA TAIFA

 KATIKA kusherehekea miaka 50 ya Uhuru ya Tanganyika, klabu ya Simba itacheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa, dhidi ya vigogo wa Ghana, Asante Kotoko Jumapili ya kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Siku hiyo, Simba SC, itashusha kikosi chake kamili, kinachohusisha nyota waliong’ara kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge mwaka huu, wakiwa na timu mbalimbali.
Hao ni pamoja na nyota walioonyesha kiwango cha juu kwenye michuano hiyo, kipa Juma Kaseja, mabeki Shomari Kapombe, Juma Jabu, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto Mwitula wa Tanzania Bara na Emanuel Okwi wa Uganda.
Lakini pia wachezaji wengine wa kigeni wa Simba akiwemo beki mpya kutoka Uganda, Derrick Walullya, kiungo Patrick Mafisango kutoka Rwanda na washambuliaji Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Felix Mumba Sunzu Jr. kutoka Zambia atakuwapo dimbani Jumapili.
Itakuwa Simba ‘full mziki’ dhidi ya mabingwa wa zamani wa Afrika,


Asante Kotoko, ambao pia ni wababe wa kihistoria wa wapinzani wao, Yanga.
Asante Kotoko ni maarufu mno Tanzania kutokana na kuitoa Yanga mara mbili mfululizo katika Klabu Bingwa Afrika mwaka 1969 na 1970 katika hatua ya Robo Fainali.
Mabingwa hao mara 20 wa Ligi ya Ghana, pia wamekuwa mabingwa wa Afrika mara mbili na kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Takwimu na Historia ya Soka, iliyo chini ya FIFA, Asante Kotoko ilikuwa klabu bora Afrika katika karne ya 20.
Imechukua ubingwa wa Afrika mwaka 1970 na 1983 na imeshika nafasi ya pili katika miaka ya 1967, 1971, 1973, 1982 na 1993, wakati lililokuwa Kombe la Washindi wamekuwa washindi wa pili mara moja mwaka 2002.
Wamechukua Kombe la FA la Ghana mara nane katika miaka ya 1958, 1960, 1976, 1978, 1984, 1989/90, 1997/98 na 2001, Kombe la Ghana SWAG mara 12 katika miaka ya 1981, 1988, 1989, 1990, 1991, 1992, 1993, 1998, 2001, 2003, 2005 na 2008 na Ghana Telecom Gala mara tatu katika miaka ya 1999/00, 2001 na 2005 na Kombe la Ghana Top Four mara mbili katika miaka ya 2003 na 2007, wakati Ghana Annual Republic Day wamebeba mara tatu katika miaka ya 2004, 2005 na 2008.


 
 Kwa upande wao Simba SC wamekuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara mara 17 katika miaka ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004 na 2007 (Ligi Ndogo) na 2010.
Kombe la Nyerere wamebeba mara tatu katika miaka ya 1984, 1995 na 2000, Ligi ya Muungano wamechukua mara tano katika miaka ya 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002, Kombe la Tusker mara nne katika miaka ya 2001, 2002, 2003 na 2005 na Kombe la Tusker Kenya mara moja 2005.
Katika mataji ya kimataifa, Simba ilikaribia kutwaa Kombe la CAF mwaka 1993 baada ya kufika fainali na kufungwa na Stella Abidjan.
Wamechukua Kombe la Kagame mara sita katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002 na walifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974.




ASANTE KOTOKO F.C:

JINA LA UTANI: Porcupines

KUANZISHWA: 1935

UWANJA WAO: Baba Yara (zamani Kumasi Sports).

MASKANI: Kumasi, Ghana

IDADI YA WATAZAMAJI: 40,000

KOCHA WAO: Maxwell Konadu

LIGIN YAO: Glo Premier League

MSIMU HUU: Wapo nafasi ya tatu



IJUE KOTOKO:

Kuanzishwa kwa Kumasi Asante Kotoko Football kunatokana na vijana 13 wa mji wa Ashanti, walioongozwa na Kwasi Kumah na ‘kupigwa tafu’ na watu wengine mashuhuri kama Kwasi Kumah, kutoka Nyankyerenease, jirani na Kumasi ambaye alikuwa Kanali wa Jeshi la kikoloni la Muingereza mjini Accra.

Akiwa mjini Accra, Kwasi Kumah alitengeneza wazo la kuanzisha klabu baada ya kushuhudia mechi kati ya Accra Standfast na Hearts of Oak. Hearts ilishinda mabao 2-1 na Sir Gordon Guggisberg, ambaye baadaye alikuwa Gavana wa Gold Coast (sasa Ghana), aliwazawadia seti ya jezi Hearts kwa soka nzuri waliyoonyesha.

Wakati Kanali Ross aliporejea nyumbani moja kwa moja na Kumah kurejea Kumasi, alinunua seti ya jezi kwa ajili ya kwenda kuanzisha timu.

Kwa ushirikiano na rafiki zake wa dhati, L.Y. Asamoah, ndipo alipoanzisha klabu inaitwa Ashanti United Football Club mwaka 1926.

Miaka mitano baadaye, ilibadilishwa jina na kuwa Kumasi Titanics na timu hiyo ilikuwa inapendwa mno kwa sababu wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa idara za serikali kama askari Magereza na Reli, ambao ilibidi wahamishwe Kumasi.

Wakitumia jina jipya la Titanics hawakuwa na bahati ya matokeo mazuri hivyo, mwaka 1934 walibadilisha jina na kutumia jina la nguvu, Mighty Atoms, ambalo pia halikuwafanya wawe tishio.

Mwaka 1935, J.S.K. Frimpong, maarufu kama Mwalimu Frimpong, aliyekuwa akifundisha shule ya serikali ya Kumasi, na ambaye alikuwa anaihusudu mno klabu hiyo na kuisaidia wachezaji aliowapika katika shule yake, alipendekeza timu hiyo ibadilishwe jina na kutoka Titanics na kuwa Kumasi Asante Kotoko Football Club. Lakini ili iwe hivyo, ilibidi wapate ruhusa kutoka kwa Mfalme wa watu wa Ashanti, Asantehene kwa sababu neno Kotoko linamaanisha Porcupine, ambayo alama rasmi ya watu wa taifa la Ashanti.

Mfalme Asantehene, Nana Sir Osei Agyeman Prempeh II, alikuwa mlezi wa kwanza wa klabu hiyo na hatimaye mwaka 1935 Kumasi Asante Kotoko Football Club ilizaliwa rasmi.

Julai mwaka huu, Asante Kotoko ilisaini mkataba wa ‘uswahiba’ na Sunderland ya Ligi Kuu ya England.

Katika mkataba huo, Sunderland watakuwa wakiisaidia Kotoko vifaa, wataalamu, katika kuendeleza mradi wa soka ya vijana kwenye klabu hiyo Ghana.

Sunderland watakuwa wakiisaidia kuwaendeleza wachezaji wa Kotoko, masuala ya tiba na kuifanya klabu hiyo ijiendeshe kibiashara.

Kikosi cha sasa Kotoko kinaundwa na makipa Isaac Amoako, Abdoulaye Soulama, George Arthur na Rashid Seidu, wakati mabeki ni Bruoma Semake, Michael Ofosu-Appiah, Henry Ohene Brenya, Prince Anokye, Louis Quainoo, Omar Gariba, Gideon Baah na Prince Boateng.

Viungo ni Stephen Oduro, Daniel Nii Adjei, Fred Brenyah, Albert Bruce na Afranie Yeboah, wakati washambuliaji ni Edward Affum, Ahmed Toure, Samad Oppong, Abdul H-Ganiyu Yahaya, David Ofei,

Wadudu Ozoro, Alex Asamoah na Seidu Traore.

Mwenyekiti wa Kotoko kwa sasa ni K.K. Sarpong, Mkurugenzi wa Mawasiliano ni Jarvis Peprah, Mkurugenzi Fedha na Utawala ni Helina Kwabbla, Mkurugenzi wa Uendeshaji Sarfo Gyamfi, Mkurugenzi wa Sheria za Ndani, Kwame Boafo, Meneja wa Timu, Opoku Afriyie na Kocha Mkuu ni Maxwell Konadu, wakati wasaidizi wake ni Emmanuel Wellington, kocha wa makipa Joseph Carr, Kocha wa mazoezi ya nguvu, Omono Asamoah Daktari Mkuu, Kwaku Boateng.

Kwa ujumla Kotoko wanakuja Tanzania kuleta burudani ya soka, lakini kuna ya kujifunza kutoka kwao, mfumo wa uendeshaji na kadhalika. Hii ni klabu ya wananchi tu kama zilivyo Simba na Yanga za hapa kwetu, tofauti ni kidogo sana.

Kwa faida ya wasomaji tu ni kwamba, logo yao ni kijani na njano kama ilivyo Yanga. Si vibaya ukiwaita Yanga wa Ghana, ambao Jumapili wataonyeshana kazi na Wekundu wa Msimbazi.

Comments