ARSENAL YANG'ARA, MAN U, CHELSEA ZADUNDWA NYUMBANI


BAO pekee la Robin Van Persie dakika ya 60, lilitosha kuwapa heri ya mwaka mpya mashabiki wa Arsenal, baada ya timu hiyo kuibukia na ushindi wa 1-0 dhidi ya Queens Park Rangers katika mchezo wa Ligi Kuu ya England kwenye Uwanja wa Emirates.
Ushindi huo, unaipandisha Arsenal hadi nafasi ya nne, baada ya kufikisha pointi 36 kutokana na mechi 19 ilizocheza.
Katika mchezo mwingine kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, Chelsea nayo ilipigwa na Aston Villa mabao 3-1 nyumbani.
Hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana 1-1, Didier Drogba akitangulia kuwafungia wenyeji kwa penalti dakika ya 23, kabla ya Ireland kusawazisha dakika tano baadaye, Petrov kupiga la pili dakika ya 83 na Bent kushindilia la ushindi dakika ya 86.
Bolton ilitoka sare ya 1-1 na Wolves, wenyeji wakitangulia kupata bao dakika ya 22 kupitia kwa Ricketts kabla ya Wolves kusawazisha dakika ya 49 kupitia kwa Fletcher.
Pia Norwich ilitoka sare ya 1-1 na Fulham. Bao la Norwich lilifungwa na Jackson dakika ya nne ya nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 90 za mchezo huo, wakati la Fulham lilifungwa na Sa dakika ya saba.
Stoke ilitoka 2 – 2 na Wigan nyumbani, mabao yake yakitiwa kimiani na Walters kwa penalti dakika ya 77 na Jerome dakika ya 84 wakati ya Wigan yalifungwa na Moses dakika ya 45 na Watson kwa penalti dakika ya 87.
Swansea City walilazimishwa sare nyumbani ya 1-1 na Tottenham, tena wakilazimika kusawazisha kupitia kwa Sinclair dakika ya 84 baada ya Van der Vaart kutangulia kuwafunga wenyeji dakika ya 44.
‘Kiboko cha Vigogo’ Blackburn jana kilizima ndoto za Manchester United kupaa kileleni mwa Ligi Kuu ya England katika mwaka mpya 2012, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Old Trafford, siku ambayo Sir Alex Ferguson alikuwa anatimiza miaka 70 tangu azaliwe.
United iliyokuwa nyuma kwa mabao 2-0, ilisawazisha kipindi cha pili kwa mabao ya Dimitar Berbatov, lakini Grant Hanley akafunga bao la ushindi katika kona dakika ya 80, akitumia vizuri makosa ya kipa David de Gea hilo likiwa bao lake la kwanza tangu atue Blackburn.
Manchester City bado wanaongoza ligi hiyo kwa tofauti ya mabao.
Ayegbeni Yakubu alipiga mabao mawili ya kwanza ya Blackburn—kwanza kwa penalti na lingine kwa shuti dhaifu akimtunga ‘kipa kimeo’ De Gea dakika ya 51.
Ligi hiyo itaendelea tena leo kwa mchezo kati ya West Brom na Everton, saa 9:30 alasiri, Sunderland na Man City saa 12:00 jioni, kesho Aston Villa itaikaribisha Swansea, Blackburn na Stoke, QPR na Norwich, Wolverhampton na Chelsea mechi zote saa 12:00 jioni, Fulham na Arsenal saa 2:30 usiku na kesho kutwa Tottenham na West Brom saa 4:45 usiku, Wigan na Sunderland saa 4:45 usiku, Man City na Liverpool saa 5:00 usiku, Newcastle na Man Utd saa 5:00 usiku na Everton na Bolton saa 5:00 usiku. 

Comments