ARSENAL YANG'ANGANIWA NYUMBANI

LONDON, England
LICHA ya kutawala mchezo kwa asilimia 64, Arsenal jana ilishindwa kuibuka na ushindi mbele ya Wolves, baada ya kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 kwenye Uwanja wa Emirates. Sare hiyo inaifanya Arsenal ifikishe pointi 33 baada ya kucheza mechi 18 na inabaki kwenye nafasi ya tano katika msimamo wa ligi, wakati Wolves imefikisha pointi 16 katika mechi 18 pia.
Mshambuliahji wa kimataifa wa Ivory Coast, Yao Gervinho aliifungia bao zuri Arsenal dakika ya nane tu ya mchezo huo, lakini Steven Fletcher  akaisawazishia Wolves dakika ya 38.
Dakika za lala salama Arsenal ilijitahidi kusaka bao la ushindi, lakini bahati haikuwa yao jana.
Krosi ya Robin van Persie dakika ya 90 na ushei iliokolewa na Kevin Doyle.
Jaribio la Van Persie tena kufunga bao dakika hiyo lilizimwa na Roger Johnson.
Kevin Doyle alimchezea rafu Yao Gervinho, lakini mpira wa adhabu uliopigwa na Mikel Arteta haukuisaidai Arsenal.
Arsenal ilishindwa hata kutumia mwanya wa Nenad Milijas  kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Mikel Arteta dakika ya 74.
Katika mchezo wa jana kikosi cha Arsenal kilikuwa; Szczesny, Mertesacker, Vermaelen, Koscielny, Djourou/Chamakh dakika ya 85,
Rosicky, Arteta, Song/Ramsey dakika ya 71, Benayoun/Arshavin dakika ya 63, Van Persie na Gervinho.
Wolves: Hennesse, Ward, Johnson, Berra, Zubar/Stearman dakika ya 50, Henry, Hunt/Doyle dakika ya 86, Jarvis, Milijas, Forde/Guedioura dakika ya 71 na Fletcher.
Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa, Liverpool wakiikaribisha  Newcastle, wakati Jumamosi Man Utd watakuwa wenyeji wa Blackburn, Arsenal na QPR, Bolton na Wolverhampton, Chelsea na Aston Villa, Norwich na Fulham, Stoke na Wigan, Swansea na Tottenham.
Man City inaongoza ligi hiyo kwa wastani wake mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ingawa kwa pointi inalingana na Man Utd, 45 kila moja na zote zimecheza mechi 18.
Tottenham ya tatu kwa pointi zake 35, ingawa yenyewe imecheza mechi 16 tu, wakati Chelsea yenye pointi 34 inashika nafasi ya nne.

Comments