YANGA SASA NI MBELE KWA MBELE

WAKATI mabingwa watetezi wa ligi kuu bara, Yanga wakianza mazoezi ya kujiwinda na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara,uongozi wa vinara hao umempa mkataba wa miezi sita, kiungo wao, Athuman Idd 'Chuji'.
Kikosi cha Yanga kimeanza mazoezi chini ya kocha wao mkuu, Mserbia Kostadin Papic, kimepania kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi hiyo na hivyo kuishia nafasi ya pili.
Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Selestine amesema kwamba kutokana na kuwa kipindi hichi ni cha lala salama, hawana budi kufanya kila linalowezekana kuhakisha wanatetea vema ubingwa wao.
"Wote mnafahamu hii ni lala salama hivyo hatuna budi kufanya maandalizi ya uhakika na hali ya juu ili kuweza kufanya vema katika michezo yetu yote na hatimaye kutetea ubingwa,"Alisema.
Mwesigwa aliongeza kuwa katika kukiimarisha kikosi chao ndiyo maana wamesajili baadhi ya wachezaji akiwemo Chuji, pamoja na kuwarejesha chipukizi wake, Omega Seme na Salum Telela ambao waliwapeleka kwa mkopo katika klabu ya Moro United.

Comments