WAWAKILISHI FC KAMBINI KESHO KUINOLEA MAKALI BUNGE FC

KIKOSI CHA BARAZA LA WAWAKILISHI
TIMU ya soka ya Baraza la Wawakilishi ya Visiwani Zanzibar kesho  inatarajiwa kuingia kambini  kujiandaa na mechi yake na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayotarajiwa kupigwa Desemba 9 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa simu kutoka Visiwani Zanzibar jana, Ofisa Michezo wa Baraza la Wawakilishi, Dau Hamad alisema kambi hiyo itakuwa katika kisiwa cha Nungwi kilicho visiwani humo, huku timu ikiwa chini ya kocha, Juma Sungi.

Alisema kwa sasa wameshaanza kujinoa kwa wachezaji kwenda na kurudi huku wakiwasubiri baadhi ya wachezaji wao ambao wapo nchini Burundi kushiriki mashindano ya Wabunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alisema katika maandalizi yao wanatarajiwa kucheza mechi moja ya kirafiki na timu ya Sharp Boys inayoshiriki ligi daraja la kwanza Visiwani humo siku chache kabla ya kuja jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, wamejipanga vema kuhakikisha wanashinda mechi yao hiyo ambapo mara ya mwisho timu hizo zilikutana Visiwani Zanzibar na timu yake kufungwa bao 1-0.

Comments