TIMBE ARUDI KWAO NA MAMILIONI YAKE

ALIYEKUWA kocha Mkuu wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Sam Timbe, ameondoka leo jijini Dar es Salaam kwenda kwao nchini Uganda, baada ya kulipwa stahiki zake alizokuwa akiudai uongozi wa klabu hiyo baada kusitisha nae mkataba wa kuinoa timu hiyo.



Ofisa habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema jana kuwa tayari wameshamlipa stahiki zake Timbe ambaye alisitishiwa ghafla mkataba na uongozi wa klabu hiyo hivi karibuni na kumrejesha kocha wake wa zamani Mserbia Kostadin Papic.
“Tumeshamalizana na Timbe kwa kumlipa kilicho chake na ameondoka jana kwenda kwao tayari kwa masuala yake binafsi,”alisema Sendeu.
Kabla ya kuondoka, juzi kocha huyo alikaririwa na gazeti hili akiapa kutoondoka mpaka atakapolipwa fedha zake baada ya kuona akizungushwa kulipwa malipo yake ambayo ni mishahara ya miezi saba na fidia ya kuvunja nae mkataba ambao ulikuwa unatarajiwa kumalizika Mei mwakani.
Hata hivyo, Sendeu hakuwa tayari kuweka wazi kiasi alicholipwa kocha huyo kwa madai kuwa ni siri baina ya uongozi na kocha huyo mwenye rekodi ya mafanikio ya kufundisha soka katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo kimeidokeza Tanzania Daima kuwa, Timbe amelipwa kitita cha shilingi milioni 36 ambazo zimejumuisha mishahara yake na fidia ya kuvunjiwa mkataba wake.

Comments