STAZ YATAKATA CHAD

TIMU ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, imejiweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2014 baada ya jana kuichapa mabao 2-1 na Chad katika mchezo wa kwanza uliochezwa mjini hapa.
Fainali za Kombe la Dunia 2014, zinatarajiwa kupigwa nchini Brazil zitakazofanyika nchini Brazil ambapo katika hatua ya makundi, Tanzania na Chad zimepangwa Kundi C lenye timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia.
Kwa matokeo hayo ya jana, Stars itahitaji sare ya aina yoyote au ushindi iliweze kutinga hatua hiyo ya makundi kwa kanda ya Afrika.
Timu itakayoibuka kidedea kati ya Tanzania na Chad baada ya mchezo wa marudiano Novemba 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ndiyo itakayoungana na timu hizo za Kundi C ambapo itakayoongoza baada ya mechi za hatua hiyo, ndiyo itakayotinga katika hatua inayofuata ya kuwania tiketi ya Brazil.
Tanzania na Chad zimelazimika kukutana katika hatua ya awali kutokana na nchi hizo kuwa miongoni mwa timu 29 ambazo kwenye viwango vya ubora vya FIFA vya Julai mwaka huu kwa Afrika, ziko chini ya timu 24 bora, hivyo kulazimika kuanzia hatua hiyo ya kuchujana zenyewe.
Hatua ya makundi inatarajiwa kuanza kuchezwa Juni 1, mwakani hadi Septemba 10, 2013, ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya fainali hizo za Dunia ambapo Afrika itawakilishwa na timu tano, huku Ulaya ikiongoza kwa kuwa na timu 13.
Kwa mujibu wa viwango vya FIFA vya Julai mwaka huu, Tanzania iko katika nafasi ya 127, wakati Chad ni ya 158.
Katika mchezo huo wa jana, Taifa Stars ndiyo iliyoanza kwa kasi na kufanya mashambulizi makali yaliyozaa bao katika dakika ya 11.
Bao hilo la Stars, lilifungwa na winga machachari wa timu hiyo, Mrisho Ngassa, lakini Chad walisawazisha bao hilo dakika moja baadaye kupitia kwa Mahamat Labo.
Bao la Chad inayonolewa na Modou Kouta, lilitokana na uzembe wa walinzi wa Stars waliozubaa kujipanga kutokana na kushangilia bao lao, hivyo wapinzani wao kutumia mwanya huo kurejesha bao hilo.
Baada ya Chad kusawazisha, wachezaji wake walitulia na kuwabana vilivyo Stars ambao waliuanza mchezo huo kwa kasi, wakipania kupata mabao ya mapema.
Kwa upande wao, wachezaji wa Stars walionekana kuchangamka zaidi katika dakika za 20 hadi 45 kwa kufanya mashambuliazi makali langoni mwa wapinzani wao kupitia washambuliaji wake, Ngassa, Thomas Ulimwengu, Shomari Kapombe na Abdi Kassim 'Babi'.
Hata hivyo, mashambulizi hayo ya Stars inayofundishwa na Mdenish Jan Poulsen, yaligonga mwamba kwa kipa wa Chad, Brice Mabaya II ambaye alikuwa imara kuokoa hatari zote zilizoelekezwa langoni mwake.
Katika kipindi cha pili, timu zote ziliianza ngwe hiyo kwa kasi kutaka kupata bao la ushindi, lakini ngome za pande zote zilikuwa ngangari kuokoa hatari zozote zilizoelekezwa langoni mwao.
Lakini alikuwa ni Nurdin Bakari aliyeipatia Stars bao la pili katika dakika ya 80 na hivyo kuihakikishia Tanzania ushindi katika mchezo huo wa ugenini.
Tanzania: Juma Kaseja, Godfrey Taita, Juma Jabu, Juma Nyoso, Aggrey Morris, Idrissa Rajabu, Thomas Ulimwengu, Abdi Kassim/Nurdin Bakari, Nizzar Khalfan, Hassan Shaaban na Shomari Kapombe.
Chad: Brice Mabaya II, Yaya Kerim, Armand Djerabe, Herman Doumna, Sylvain Doubam, Hassan Hassan, Karl Barthelemy/Djingabeye Appolinaire, Mahamat Labo/Rodrigue Casimir, Ezechiel Ndouasel, Massama Asselmo/Cesar Abaya na Ferdinand Gassina.
Timu nyingine zilizshuka dimbani jana kuwania kutinga hatua ya makundi, ni Somalia iliyopambana na Ethiopia, Guinea ya Ikweta na Madagascar, Lesotho dhidi ya Burundi, Sao Tome e Principe na Kongo, Shelisheli na Kenya, Djibouti dhidi ya Namibia, wakati Comoro ilikuwa ikimenyana na Msumbiji.
Eritrea iliikaribisha Rwanda, Guinea-Bissau dhidi ya Togo, wakati Swaziland ilipambana na DR Congo, huku Mauritius ikionyeshana kazi na Liberia.

Comments