MRWANDA ATEMWA STARS, BOCCO ACHUKUA NAFASI

WAKATI kikosi cha timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kimeingia kambini leo kujiandaa na mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena, kocha wa timu hiyo Jan Poulsen amemtema mshambuliaji wa Kimataifa Dan Mrwanda na kumuita mshambuliaji wa Azam, John Bocco ‘Adebayor’.

Poulsen  amemua kumuacha mchezaji huyo anayekipiga katika klabu ya DT Long An, Vietnam kutokana na kutokuwa na uhakika kama atajiunga na wenzake kwa wakati kwani muda kujiandaa kabla ya mechi hiyo ni mdogo.
Stars inatarajiwa kuondoka nchini kwenda Chad Novemba 9 kwa ajili ya mchezo huo kabla ya kurudiana Novemba 15 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wengine walioitwa katika kikosi hicho ni pamoja na Makipa, Juma Kaseja (Simba), Mwandini Ally (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Juma Nyoso (Simba), Idrissa Rajab (Sofapaka, Kenya), Erasto Nyoni (Azam), Nadir Haroub (Yanga), Godfrey Taita (Yanga) na Juma Jabu (Simba).
Viungo ni Henry Joseph (Kongsvinger IL, Norway), Nurdin Bakari (Yanga), Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Abdi Kassim (DT Long An, Vietnam), Ramadhan Chombo (Azam) na Shomari Kapombe (Simba).
Washambuliaji katika kikosi hicho ni Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada), Mrisho Ngassa (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Athuman Machupa (Vasalund IF, Sweden), Hussein Javu (Mtibwa Sugar) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC).
Katika hatua nyingine, wadhamini wa Stars, benki ya NMB jana imemwaga vifaa mbalimbali kwa timu hiyo vyenye thamani ya shilingi milioni 9.

Comments