'HATUJAMFUKUZA BASENA'

Kamati ya Utendaji haikumjadili Moses Basena wala kuchukua maamuzi yoyote kumhusu. Hii inatokana na ukweli kwamba Simba SC ni klabu ya kistaarabu na inafahamu kuwa kocha wake huyo yuko kwenye msiba mzito wa mama yake mzazi.
Klabu ya Simba inapenda kutumia nafasi hii kukanusha habari zote kuhusu kusimamishwa au kufukuzwa kazi kwa Basena katika kipindi hiki kigumu kwake.

WACHEZAJI WA TIMU YA VIJANA YA SIMBA:
Kama inavyofahamika, Simba imesajili wachezaji 26 kwa ajili ya Ligi Kuu ya Vodacom msimu huu ingawa Kanuni za TFF zinaruhusu timu kusajili wachezaji wasiozidi 30.
Kamati ya Utendaji imeamua kuwa nafasi nne zilizobaki (ili kufikia 30) zitajazwa na wachezaji kutoka timu za vijana za Simba.
Majina ya wachezaji hao yatapatikana baada ya Kamati ya Ufundi na Benchi la Ufundi kukutana na kujadiliana kuhusu wachezaji watakaofaa kwa ajili hiyo.
Simba ni timu ambayo falsafa yake ya soka inafahamika. Wachezaji ambao wamepikwa ndani ya timu (kama hao wa timu za vijana) wanafundishwa kwenye falsafa hiyo na wanatarajiwa kuwa mabalozi wazuri wa falsafa ya klabu.
Klabu maarufu na zenye mafanikio duniani kama vile Barcelona na Man United zimefanikiwa sana kwa kukuza vipaji kutoka kwenye timu zake za vijana.
Simba inaelekea kwenye njia hiyo.

VURUGU VIWANJANI:
Kamati ya Utendaji ya Simba imesikitishwa sana na vitendo vya vurugu vilivyofanywa na baadhi ya washabiki wake wakati wa mchezo wa mwisho wa raundi ya kwanza ya Ligi Kuu dhidi ya Moro United.
Washabiki hao wachache walikuwa wakitoa lugha ya matusi, vitisho na vurugu dhidi ya wachezaji na viongozi wa Simba waliokuwapo uwanjani.
Kamati iliazimia kuwa wakati umefika sasa kwa vyombo vya dola kushughulikia washabiki wanaofanya vitendo visivyo vya kiungwana katika viwanja vya soka nchini.
Kwa taarifa hii, Simba inawaomba washabiki wake waendelee kuwa alama ya uungwana na ustaarabu michezoni. Washabiki wa Simba wanafahamika kote duniani kwa sifa hii.
Simba SC haitatetea mpenzi au mwanachama wake yeyote atakayekutwa na hatia ya kufanya vitendo vya vurugu uwanjani.

Comments