FEDHA ZA MOSHA ZAZUA KIZAA ZAA YANGA


Na Dina Ismail
ALMANUSRA zoezi la  kuwatunuku wachezaji wa Yanga kutokana na kuwafunga mahasimu wao Simba,kutoka kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davies Mosha, iingie dosari baada ya uongozi kuzuia zoezi hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa uongozi ulitaka ukabidhiwe fedha hizo. 
Kama hiyo haitoshi, waandishi waliohudhuria hafla hiyo walishuhudia viti vikitolewa katika ukumbi hiyo bila kuelezwa sababu ya zoezi hilo.
Lakini uchunguzi unaonyesha kwamba, mwnyekiti wa timu hiyo ambaye amekuwa na msigano wa muda mrefu ambao ulipelekea Mosha kujiuzulu, ndiye alielekeza zoezi hilo ambalo hata hivyo halikufanmikiwa baada ya kubaini waandishi kushtukia picha yote.
Hata hivyo baada ya mvutano, uongozi ulisalimu amri ambapo Mosha kupitia mwakilishi wake, Abek Mcharo alitoa kitita cha  shilingi mili.10  ikiwa ni katika kutimiza ahadi yake ya kuwatunuku wachezaji wa timu hiyo kutokana na kuwafunga mahasimu wao wa jadi, Simba bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu ya Vodacom jumapili iliyopita.
Fedha hizo zilikabidhiwa na mwakilishi wa Mosha, Abel Mcharo kwa kocha wa Yanga, Kostadin Papic katika hafla fupi iliyofanyika makao makuu ya klabu hiyo mitaa ya Jangwani na Twiga.
Katika salamu zake kwa wachezaji wa timu hiyo, Mosha alisema kwamba kama mwanachama wa Yanga hana budi kutekeleza ahadi aliyoitoa kabla ya mchezo huo ambao alishindwa kuushuhudia kutokana na kikazi nje ya nchi.
“Nasikitika kwamba sikuweza kuhudhuria katika pambano hilo kutokana na kuwa nje, nimerejea jana (juzi)  lakini kwa kuwa muungwana ni vitendo nikaona nitekeleze ahadi yangu,”Alisema.
Mosha alieleza kuwa tukio hilo lisionekane vinginevyo kwani siku za nyuma aliahidi kuendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa klabu hiyo pamoja na kushirikiana katika mambo yote yenye kuleta maendeleo na tija.
“Lakini kuelekea utekelezaji wa ahadi yangu, mengi yamezungumzwa na hata kuripotiwa kwenye vyombo vya habari, napenda kusema kuwa kwenye wengi hapakosi mengi, nawaasa Wanayanga wenzangu kuwa huu si wakati wa kuangalia tulikotoka, ila ni wakati wa kuangalia tulipo na  tunapoelekea, yote ni kwa maslahi ya Wanayanga”, Aliongeza.
Aidha, Mosha alisema hayo anayoyafanya kwa wachezaji si kwa manufaa au faida yake bali kwa ajili ya mshikamano wa Wanayanga wote.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa klabu hiyo, Mjumbe wa kamati ya Utendaji na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya ufundi, Ali Mayai alishukuru kwa kitendo hicho cha Mosha, huku akiwataka wadau wengine kuungana naye ili kuzidi kuwapa morali wachezaji.

Comments