FAINANI UHAI CUP YASOGEZWA HADI KESHO

Mechi ya fainali ya michuano ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Kombe la Uhai (Uhai Cup) kwa klabu za Ligi Kuu sasa itachezwa kesho (Novemba 26 mwaka huu) saa 3.00 asubuhi kwenye Uwanja wa Karume.
Awali fainali hiyo kati ya Simba ambayo iliingia hatua hiyo kwa kuitandika Toto Africans mabao 4-1 na Azam iliyofuzu kwa kuizamisha Serengeti Boys (timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17) mabao 3-0 ilikuwa ichezwe leo (Novemba 25 mwaka huu) saa 9.00 kwenye uwanja huo.
Mabadiliko hayo yamefanyika ili kutoa nafasi kwa mashabiki kushuhudia mechi za michuano ya Kombe la Chalenji inayoanza leo (Novemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa. Kila siku kwenye michuano ya Chalenji zinachezwa mechi mbili; ya kwanza saa 8.00 mchana na nyingine saa 10.00 jioni.
Michuano ya Kombe la Uhai inadhaminiwa na Kampuni ya S.S. Bakhresa kupitia maji Uhai ambapo bingwa atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000. Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba.
Mchezaji bora sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu sh. 300,000.

Comments