BASENA HAKUWA NA VYETI:SIMBA

WEKUNDU wa Msimbazi, Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imefafanua kuwa iliamua kuvunja mkataba na aliyekuwa kocha wake mkuu, Mganda Moses Basena, kutokana na kocha huyo kutokuwa na vyeti vya taaluma yake kama kanuni na sheria za soka zilivyoainishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pamoja na zile za nchi.

Hivi karibuni, Simba ilivunja mkataba na Basena aliyedumu na timu hiyo kwa takriban miezi sita, ambapo nafasi yake imechukuliwa na Mserbia aliyepata kuinoa timu hiyo mwaka juzi kabla ya kutimka, Milovan Cirkovic.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, hadi kufikia hatua ya kuvunja mkataba na Basena walikwisha kuchoshwa na kocha huyo kutowasilisha vyeti vyake, kama alivyoahidi mara baada ya kuwepo makubaliano ya kuinoa timu yao.

Alisema pamoja na kukosa vyeti hivyo, pia walikuwa wakisumbuliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani kila wakati, kutokana na ukweli kuwa ingekuwa vigumu kocha huyo kupewa kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini bila ya kuwa na vyeti halali vya fani yake.

“Wengi hawajui, lakini sababu kubwa ya kuachana na Basena ni kutotuletea nakala halisi ya vyeti vya taaluma yake kama zinavyoelekeza kanuni za TFF, hata Uhamiaji walikuwa wakitusumbua mara kwa mara kuhusiana na hilo, hatukuwa na jinsi ndiyo maana tukaona tuvunje mkataba,” alisema.

Akizungumzia mustakabali mzima wa Milovan, Kaburu alisema, kocha huyo ambaye anaanza rasmi kibarua chake leo, amepewa mkataba wa miezi sita, ambao utakuwa katika uangalizi na kama ataweza kuiweka timu katika kiwango cha juu, watampa mkataba wa kudumu utakaokuwa kati ya mwaka mmoja hadi miwili.

“Kwa sasa Milovan tumempa miezi sita ya uangalizi kwanza, kama tutaridhishwa na utendaji wake, tutakaa chini na kumpa mkataba wa muda mrefu, sisi tunataka kocha ambaye ataipatia mafanikio timu na si bora kocha,” alisema Kaburu.

Comments