BAADA YA KUSAFISHWA...WAMBURA AICHAMBUA TFF

ALIYEKUWA Mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha soka mkoa wa Mara (FAM) Michael Richard Wambura, ameibuka na kusema kuwa kitendo cha kushinda rufaa yake ni kilelezo tosha kuwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limepoteza mwelekeo wa kusimamia soka nchini.
Wambura aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam leo katika mahojiano maalum na kituo cha Luninga cha TBC 1, ambapo alisema kitendo cha kamati ya rufaa kumpa haki yake kimeweza kumsafisha mbele ya jamii hasa katika medani ya soka.
“Pamoja na kushinda rufaa yangu lakini bado ninapenda ieleweke kuwa haya niliyofanyiwa ni mizengwe ya hali ya juu dhidi yangu na katika hili ninajua huenda kulikuwa na kundi kubwa la watu likinyimwa haki zao na TFF kwa sababu tu ya maslahi ya kundi fulani,” alisema Wambura.
Wambura ambaye, kwa nyakati tofauti aliwahi kuwa katibu Mkuu wa Simba na FAT, alisema mchezo wa soka hivi sasa umekuwa ukipoteza mwelekeo kuanzia ngazi za mikoa hali inayochangiwa na viongozi wa TFF kushindwa kuwa wabunifu na kutafuta njia mbadala na ya dhati ili kuweza kuliinua.
Alisema hatua ya yeye kuzuiwa kugombea nafasi ya Uenyekiti katu haimzui kutoa mchango wake huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa viongozi waliochaguliwa na asingependa uongozi huo uvunjwe kutokana na kushinda rufaa yake.
“Nilipokuwa Katibu mkuu wa FAT hali ilikuwa tofauti sana, na hata pindi kama ndoto yangu ikifanikiwa ya kuiongoza TFF ya sasa kuna kazi ya kuvunja makundi hasa kuanzia katika utawala, hata Katibu Mkuu wa TFF anaonekana kuwa ni mtu wa nani badala ya kuwa kiongozi wa kila mtu.
“Hata nilipopeleka fomu yangu ya rufaa TFF nina hakika kuna viongozi walikuwa wakitoa maelekezo …. Kila ofisa hata mfagiaji wa ofisi alikuwa hataki kunisogelea kwa hofu ya kufukuzwa kazi na mtu fulani,” alisema Wambura.
Alisema kutokana na hali hiyo kumelifanya soka la bongo kuingia katika mgogoro unaosababishwa na viongozi wa ngazi ya juu ya TFF kwa kuwa na makundi ambayo yanazingatia maslahi yao binafsi kuliko ya soka.
“Nilipokuwa Katibu Mkuu wa FAT, wadau walikuwa wakitoa maoni yao akiwemo ya Rais wa sasa wa TFF Leodger Tenga, kupitia Manispaa ya Temeke kama mdau, lakini hivi sasa toka ameingia madrakani chombo hiki imekuwa ni mali ya watu wachache na maoni ya wadau hakuna tena je hili limeishia wapi au ndiyo zilikuwa hila za kujiandaa kwake kupata uongozi,” alihoji Wambura.
Wambura, alisema kutokana na hali hiyo yamejengwa mazingira hadi kwa wajumbe ambapo wengi wao wamekuwa waoga kusema ukweli katika mikutano mikuu kwa kuhofia kushulikiwa pindi uchaguzi unapowadia.
Juzi kamati ya rufaa ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Profesa Mgongo Fimbo, ilimsafisha Wambura ambaye alikata rufaa baada kuenguliwa kugombea FAM kwa madai ya kutokuwa muadilifu na hivyo kuenguliwa kugombea katika uchaguzi huo.

Comments

  1. YANGA BOMBA-UHURU BRANCHNovember 27, 2011 at 6:52 PM

    TANZANIA KWA VITUKO!MICHAEL SASA NAYEYE ANATAKA KUJIFANYA KAMA LOWASSA WA KWENYE SOKA SIO!NAONA KAIBUKA UPYA!

    ReplyDelete

Post a Comment