AZAM FC YAFAGILIWA BUNGENI

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenela Mukangara, ameifagilia bungeni Kampuni ya SS Bakhresa inayomiliki timu ya soka ya Azam FC, kwa hatua yake ya kujenga uwanja wa kisasa eneo la Chamazi, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Dk. Mukangara, alitoa pongezi hizo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), aliyehoji idadi ya viwanja bora vya michezo vilivyopo nchini na wamiliki wake.
“Nachukua nafasi hii kuipongeza Klabu ya Azam kwa kujenga kiwanja chao cha kisasa, ikiwa ni kutekeleza kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), zinazovitaka vilabu kuwa na viwanja vyake vya michezo,” alisema Dk. Mukangara.
Katika ufafanuzi wa swali hilo, Dk. Mukangara alisema, viwanja vilivyopo sasa vinavyomilikiwa na serikali, halmashauri na klabu mbalimbali ni 27, ambavyo vimegawanywa katika madaraja manne.
Kuhusu umiliki wa viwanja hivyo, Mukangara alisema kuwa, serikali kuu inamiliki viwanja viwili, halmashauri 10, Chama cha Mapinduzi (CCM), 12 na vilivyosalia vitatu vinamilikiwa na Klabu za Yanga, Mtibwa na Azam.

Comments