YANGA WASHTUKA, WAKATISHA MAPUMZIKO

MABINGWA watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Yanga wamefuta mapumziko ya siku tatu waliyowapa wachezaji wake na hivyo kuendelea kujifua kwa ajili ya kujiandaa na ligi hiyo. 
Yanga ambayo katika katikati ya wiki hii ilipata ushindi mnono kwa kuilamba Coastal Union ya Tanga kwa mabao 5-0, iliamua kuwapa mapimziko wachezaji wake huku ikipanga kuanza kujinoa jumatatu, lakini jana ilisitisha mapumziko hayo. 
Msemaji wa Yanga Louis Sendeu alisema jana kwamba wameamua kusitisha mapumziko hayo kutokana na timu kukabiliwa na ushindani mkubwa wa ligi katika mechi zinazofuata. 
Alisema ushindi walioupata umewapa changamoto ya kujiandaa zaidi ili kuweza kukabiliana na ushindani wa mechi zinazofuata kwani kila timu imeingiwa na wasiwasi kutokana na kipigo hicho.

Sendeu aliongeza kuwa katika siku ambazo ligi hiyo imesimama wachezaji watakuwa wakifanya mazoezi asubuhi tu katika uwanja wa Taifa, hivyo anaamini timu yake itaendelea kufanya vema katika ligi hiyo.
 “Unajua timu yetu ilianza vibaya ligi,lakini taratibu ilianza kuimarika mpaka kupata ushindi ule mnono, sasa ni lazima kuna timu zitaingiwa na kujiandaa vema, tumeona heri tuachane na mapumziko na tuendelee kujiandaa,”Alisema.
 Alisema, kikosi cha Yanga kwa sasa kipo chini ya kocha msaidizi, Fred Felix Minziro ambaye anakaimu mikoba ya Mganda Sam Timbe aliyekwenda kwa mapumziko mafupi ambapo anatarajiwa kurejea kesho.

Comments