YANGA NA POLISI KESHO KAUNDA

KIKOSI cha Yanga kinatarajia kushuka uwanjani kesho kucheza mchezo wa kirafiki na Polisi ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Kaunda, Jijini. Mechi hiyo itampa nafasi kocha mkuu wa timu hiyo, Mganda Sam Timbe, kujua mapungufu katika kikosi chake kabla ya mechi yao ya Oktoba 14 mwaka huu, dhidi ya Kagera Sugar, itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Akizungumza na DIMBA jana, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema mechi hiyo itakuwa ni maalumu kwao kwa ajili ya kikosi chao na kwa Polisi, ambayo wachezaji wake wengi Oktoba 15 mwaka huu, wataanza kampeni za kupanda kucheza Ligi Kuu katika michuano ya Ligi Daraja la Kwanza msimu huu. “Utakuwa ni muda mzuri kwa kocha kuangalia mapungufu katika kikosi chake, ni mechi ambayo imeandaliwa na benchi la ufundi kwa ajili ya maandalizi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, katika mechi tano zilizosalia za mzunguko wa kwanza,” alisema Sendeu. Alisema baada ya mchezo wa leo, timu yao itaendelea kujinoa kwa ajili ya kusubiri mechi yao inayokuja dhidi ya Kagera. Timu za jeshi zimekuwa zikiisumbua Yanga ambao katika mechi zao za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, walianza kwa kufungwa na JKT Ruvu bao 1-0 na wakatoa sare ya bao 1-1 na Ruvu Shooting.  Yanga watakuwa na kibarua kingine kutoka kwa Maafande wa JKT Oljoro Oktoba 23 mwaka huu, na Polisi Dodoma Novemba 5.  Sendeu alisema katika mchezo wa leo, kiingilio kitakuwa Sh 3,000 kwa watazamaji watakaokaa ghorofani na mzunguko ni Sh 2,000.

Comments