WACHEZAJI YANGA WAGOMEA MAZOEZI YA ASUBUHI WAKISHINIKIZA KULIPWA MISHAHARA YAO

WAKATI ijumaa  Yanga inatarajiwa kushuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam kukwaana na Kagera Sugar, wachezaji wa timu hiyo jana waligoma kufanya mazoezi wakishinikiza kulipwa mishahara yao kuanzia mwezi Septemba, imefahamika.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kwamba wachezaji hao waliamua kuendesha mgomo huo baada ya kupigwa danadana za mara kwa mara na viongozi wa klabu hiyo kuhusiana na mustakabali mzima juu ya ulipwaji wa mishahara yao.
Kama hiyo haitoshi wachezaji hao walipinga kambi yao kuwa katika klabu yao iliyopo mitaa ya Jangwani na Twiga kwa madai kwamba mifumo ya kupandisha maji katika vyumba wanavyolala haifanyi kazi.
Habari zinaongeza kuwa, kufuatia hali hiyo, uongozi wa Yanga ilibidi ukae kikao na wachezaji hao ili kuweza kufikia muafaka kuhusiana mustakabali mzima wa mgomo huo.
Alipotafutwa msemaji wa Yanga Louis Sendeu kuzungumzia kitendo hicho, alisema kuwa “Hizo ni propaganda tu ambazo ni za kupuuzwa,si kweli leo wachezaji asubuhi hawakufanya mazoezi kwa sababu uwanja wetu ulijaa maji, lakini jioni walifanya mazoezi kama kawaida kabla ya kuingia kambini,”.
Kuhusiana na kikao baina yao na wachezaji, Sendeu alisema kuwa kilikuwa cha kawaida katika kupeana mikakati ya kuelekea katika mechi hiyo na michezo mingine iliyobaki katika ligi kuu soka Tanzania Bara.
Hata hivyo taarifa zinadai kuwa uongozi umewalipa wachezaji hao stahiki zao na kukukubali kuingia kambini klabuni hapo, huku pia mafundi wakianza kurekebisha mifumo ya maji.

Comments