T-MOTO WAMPIGA MKWARA MWANAHAWA ALLY




KUNDI jipya la muziki wa taarab la TanzaniaModern Taarab ‘T-Moto’, limemzuia msanii wake, Mwanahawa Ally kupanda jukwaani katika maonyesho ya kundi la muziki huo la Five Stars na mengineyo.
Msanii huyo mwishoni mwa wiki alitajwa kuwa miongoni mwa watakaoimba wakati wa onyesho la Five Stars jijini Dar es Salaam, lakini alishindwa kufanya hivyo baada ya kugomewa na uongozi wa T-Moto.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa T-Moto, Amin Salmin ‘Mourinho’, wamemzuia Bi Mwanahawa kupanda jukwaani katika maonyesho ya Five Stars kwa kuwa ana mkataba na kundi lao.

Alisema kuwa wiki iliyopita walisikia kuwa msanii wao huyo atakuwapo wakati wa shoo ya Five Stars Ijumaa iliyopita kwenye Ukumbi wa Mashujaa Pub uliopo Vingunguti, Dar es Salaam , hivyo waliwasiliana naye na kumzuia kufanya hivyo.

“Bi Mwanahawa ana mkataba na T-Moto, hivyo hawezi kupanda katika jukwaa la kundi lolote lile bila ridhaa ya ya kundi lake, tulishangaa kusikia anatajwa kupanda jukwaani katika shoo ya Five Stars, tulimzuia na hakufanya hivyo,” alisema Salmin.

Hata hivyo, alisema wamemruhusu msanii huyo kupanda jukwaani katika maonyesho ya kundi la Melody Modern Taarab kwa wakati huu wanaposubiri kuzindua kundi lao, Oktoba 30, mwaka huu.

Baada ya kupata usajili rasmi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), ikiwa ni pamoja na kupata kibali cha kujihusisha na sanaa hiyo ndani na nje ya nchi, T-Moto wamepania kufanya kweli na kuvifunika vikundi vyote vya taarab nchini.

Tayari kundi hilo limeshaingia Studio za Bakunde Production zilizopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam kurekodi nyimbo zake mpya zilizokamilika ili kukamilikamisha albam yao ya kwanza itakayojulikana kwa jina la Aliyeniumba Hajanikosea.

Mbali ya Bi Mwanahawa, wasanii wengine wanaounda kundi hilo ni kiongozi Jumanne Ulaya ‘Mkono wa Biashara’, Jokha Kassim, Mrisho Rajab, Musa Mipango, Hassan Ally, Mosi Suleiman, Rajab Kondo, Fadhili Mnara,Moshi Mtambo, Ally Kabura, Sabha, Rahma, Asha Masanja na Hanifah Kasim na wengineo.
Nyimbo za kundi hilo ambazo zimeshakamilika ni Aliyeniumba Hajanikosea uliobeba jina la albam ambao umeimbwa na Mwanahawa, ‘Unavyojidhani Mbona Hufanani’ (Jokha), ‘Mtoto wa Bongo’ (Hassan Ally), ‘Mchimba Kaburi Sasa Zamu Yake Imefika’ (Rajab), ‘ Mwenye Kustiri Mungu’ na ‘Kumbe Wewe ni Shoti’ (Mosi) na ‘Riziki na Shortcut’ (Aisha).

Comments