SIMBA KUPOZA MACHUNGU KWA MORO UNITED J'TANO

UONGOZI wa vinara wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba, umesema kwamba umejipanga kuhakikisha timu yake inashinda mechi yao ya keshok utwadhidi ya Moro United itakayofanyika kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ili kupunguza machungu ya kipigo walichokipata Jumamosi kutoka kwa watani zao Yanga.
Simba ambayo inaongoza ligi ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga katika mchezo uliofanyika Jumamosi na kuharibu rekodi yao ya kutopoteza mechi hata moja tangu kuanza kwa msimu huu wa mwaka 2011/ 2012.
Makamu Mwenyekiti wa timu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu', amesema kwamba wachezaji wao waliingia kambini juzi na jana walianza mazoezi kwa ajili ya kuivaa Moro United huku kila mchezaji akiahidi kufanya vizuri katika mechi hiyo ili kurejesha matumaini ya kutwaa ubingwa wa ligi ambao unashikiliwa na watani zao.
Kaburu alisema kwamba kupoteza mechi hiyo ya juzi sio mwisho wa ligi na hakujawachanganya na wote wamerejesha nguvu zao katika mechi ya kesho na nyingine za mzunguko wa pili zitakazoanza mapema mwezi Januari hapo mwakani.
"Ligi bado inaendelea na kufungwa mechi moja ni sehemu ya mchezo, tumejipanga kuhakikisha tunashinda mechi ya Moro United ingawa tunafahamu kwamba haitakuwa nyepesi," alisema.
Aliongeza kuwa katika mchezo huo wa kesho Simba itawakosa Jerry Santo na Emmanuel Okwi ambao wanakadi za njano pamoja na beki, Nassor Saidi 'Chollo' ambaye anasumbuliwa na maumivu ya nyama za misuli aliyoyapata katika mechi ya Yanga na kumfanya atolewe nje.
Alisema kuwa Kamati ya Utendaji ya Simba ilitarajiwa kukutana jana jioni kujadili mambo mbalimbali ikiwemo ripoti kutoka kwa Kamati yake ya Ufundi ambayo ilikutana juzi.
Moro United imesharejea jijini ikitokea Manungu mkoani Morogoro na itashuka kuikabili Simba ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha magoli 3-1 walichokipata kutoka kwa Mtibwa Sugar.
Wekundu wa Msimbazi ndio wanaongoza ligi kwa kuwa na pointi 27 wakifuatiwa na Yanga wenye pointi 24 na kesho wenyewe watakuwa mkoani Dodoma kuwavaa Polisi ya huko kwenye uwanja wa Jamhuri.

Comments