MANJI AWAAHIDI DONGE NONO WACHEZAJI WA YANGA WAKISHINDA MECHI ZILIZOBAKI

WACHEZAJI wa Yanga wameingiwa mchecheto baada ya kuahidiwa donge nono na mfadhili wao Yusuf Manji iwapo watashinda mechi zao zilizobaki katika ligi kuu soka Tanzania Bara.



Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema kwamba, Manji ambaye anatarajiwa kusaini mkataba mpya wa ufadhili wa klabu hiyo wakati wowote kuanzia sasa amewaaahidi wachezaji kitita hicho ili kutoa motisha ya kufanya vema.


Alisema Manji ambaye anatarajiwa kuwasili leo kutoka nchini Marekani, ametoa mikakati hiyo alipowasiliana na uongozi wakati walipomtaka arejee kuifadhili timu hiyo ili kurejesha hadhi yake ambayo tangu kujiondoa kwake imekuwa na mwenendo usioridhisha.


“Unajua Manji anapenda sana timu ifanye vizuri ndiyo maana katika moja ya ahadi zake alizozitoa pindi atakaporejea tena kutufadhili ni kutoa donge nono kwa wachezaji iwapo watashinda mechi zilizosalia kwenye ligi,”Alisema.


Juzi, mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga aliwaambia waandishi wa habari kwamba uongozi umeamua kumuangukia Manji aliyekuwa akiifadhili siku za nyuma kabla ya kujiondoa kutokana na msigano uliokuwepo baina yake na wanachama, wakimtaka kurejea tena.


Nchunga alisema, mazungumzo hayo yamefikia vizuri na pindi atakaporejea kutoka Marekani anatarajiwa kusainia mkataba mpya wa kuifadhili klabu hiyo ambayo imekumbwa na ukata tangu kujindoa kwake ambapo juzi wachezaji waligoma wakishinikiza walipwe mishahara yao ya mwezi Septemba.


Yanga ambayo inashika nafasi ya sita kwenye ligi hiyo leo itashuka katika Uwanja wa Taifa kukipiga na Kagera Sugar ambapo pia imebakiwa na mechi baina ya timu za Toto African, JKT Oljoro, Simba na Polisi Dodoma.

Comments