MAKALI YA JULIO YAANZA KUONEKANA COASTAL, YAITANDIKA VILLA SQUAD 6-1

‘Wagosi wa Kaya’ Coastal Union ya huko leo wameona mwezi baada kuwatandika vibonde wenzao kwenye ligi hiyo, Villa Squad kwa mabao 6-1.

Katika mechi hiyo iliyopigwa kwenye dimba la Mkwakwani, Tanga, mabao ya Coastal yalifungwa na Busungu Francis aliyeandika la kwanza na la pili, Said Sued aliyefunga la tatu na la nne, huku bao la tano likifungwa na Mwandawa Rashid na Salum Aziz Gilla alifunga la sita, wakati Mohammed Kijuso aliifungia Villa bao pekee.
Ushindi huo mkubwa kwa Wagosi hao umetiwa chachu na kocha mpya aliyepewa mikoba ya kukisuka kikosi hicho kilichoanza kupoteza mwelekeo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ambaye ameahidi kuibadilisha timu hiyo kutoka ilipokuwa hadi kuwa tishio.
Kwa ushindi huo, Coastal iliyokuwa ikishikilia mkia kwa kuwa na pointi nne sasa imepanda hadi nafasi ya pili kutoka mwisho baada ya kufikisha pointi saba, huku Villa ambayo ilikuwa inashika nafasi ya pili kutoka mwisho ikishuka mpaka mkiani, kwani imebaki na pointi zake sita.
Katika hatua nyingine, Kagera Sugar imeifunga African Lyon bao 1-0 kupitia mchezo wao uliopigwa kwenye dimba la Chamazi jijini Dar es Salaam.

Comments