JKT OLJORO YAIPUMULIA SIMBA LIGI KUU

TIMU iliyopanda  ya JKT Oljoro  imepanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara baada ya kuifunga Coastal Union ya Tanga kwa bao 1-0, mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Ushindi wa maafande hao umeifanya ifikishe pointi 16 hivyo kupanda hadi nafasi ya pili nyuma ya vinara wa ligi hiyo Simba yenye pointi 18 huku Azam ikishuka hadi nasafi ya tatu wakiwa na pointi 15.
Aidha, Mtibwa Sugar nayo imeifunga Ruvu Shooting mabao 2-1, ambapo ushindi huo unaipandisha hadi nafasi ya nne kutoka ya tano baada ya kufikisha pointi 15 na hivyo kuishusha Yanga yenye pointi 12 katika nafasi ya tano.
Katika hatua nyingine, kwenye dimba Chamazi ambapo Villa Squad na Moro United zilimaliza kwa sare ya bao 1-1.
Villa ndio walikuwa wakwanza kufunga bao katika dakika ya 18 lililofungwa na Nsa Job kwa mkwaju wa penati iliyotokana na mabeki wa Moro kumkwatua ndani ya eneo la hatari.
Baada ya bao hilo Villa waliendelea kulisakama lango la Moro lakini mabeki wake walikuwa makini na kuondosha hatari langoni mwao, bao lililodumu hadi kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili Moro walirejea uwanjani wakiwa na nguvu mpya na kulisakama lango la Villa na kufanikiwa kufunga bao katika dakika ya 89 lililofungwa na Omega Seme kwa mkwaju mkali kutoka nje kidogo ya eneo hatari na kujaa wavuni.
Aidha, Toto Africa ya Mwanza ilikuwa mgeni wa Polisi Tanzania ambapo kupitia mchezo wao uliopigwa kwenye dimba la Jamhuri mkini Dodoma, timu hizo zilitoka sare tasa.

Comments