ANGOLA, GHANA ZAFUZU AFCON, GHANA CHALI



LAGOS, Nigeria


NIGERIA imetupwa nje ya michuano hiyo baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nyumbani dhidi ya Guinea, matokeo yanayowaacha wakimaliza mechi hizo za kufuzu wakiwa katika nafasi ya pili ya kundi B wakiwa na pointi 11 nyuma ya vinara Guinea wenye pointi 14. Nigeria wanasubiri majaliwa ya mshindi wa pili bora.


Katika mchezo huo Guinea walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Ismael Bangura, baada ya bao hilo Nigeria walikuja juu na kusawazisha kupitia kwa Obinna Nsfor, aliyepiga shuti kali akiwa nje ya eneo la hatari na kufanya matokeo kuwa 1-1. Nigeria waliendelea kushambulia lango la Guinea na kufanikiwa kufufua matumaini ya kufuzu baada ya Ikechukwu Uche kuifungia bao la pili.


Guinea walionekana wamepania kuhakikisha Nigeria hawanusi kwenye mashindano ya mwakani baada ya Ibrahima Traore kuifungia bao la pili na akimalizia mchezo mzuri wa timu yake na kufanya matokeo kuwa 2-2 yaliyodumu hadi mwisho wa mchezo na kushudia Nigeria wakikutwa na dhahama hiyo ya kukosa michuano ya mwakani.


Nigeria wanaungana na Misri na Cameroon katika orodha ya mataifa makubwa katika soka ambayo yameshindwa kufuzu moja kwa moja kwa ajili ya michuano ya mwakani ya Afrika.


Katika michezo mingine Angola imefuzu kushiriki fainali za kombe la mataifa ya Afrika baada ya kuilaza Guinea Bissau mabao 2-0, huku waliokuwa vinara wa kundi hilo Uganda waking’ang’aniwa na Kenya nyumbani na kutoka sare ya 0-0.


Uganda hawawezi kupata nafasi ya mshindi wa pili bora na Kenya ambao wameibania Uganda pia hawana nafasi ya kushiriki michuano hiyo, Uganda ilikuwa inahitaji ushindi kujihakikishia kushiriki fainali za mwakani nchini Gabon na Guinea ya Ikweta, lakini walishindwa kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani na nafasi za wazi walizotengeneza.


Kwa upande wa Ghana wamejihakikishia kufuzu kwa ajili ya michuano hiyo baada ya kuilaza Sudan kwa mabao 2-0 mabao ya Ghana yaliwekwa kimiani na mchezaji bora wa Afrika wa BBC, Asamoah Gyan, katika dakika ya 10 ya mchezo huo huku bao la pili likifungwa na John Mensah bao lililoihakikishia Black Stars nafasi ya kufuzu kwa ajili ya fainali za michuano hiyo.


Matokeo katika mechi nyingine zilizokuwa zimekwisha wakati tukienda mtamboni yalikuwa kama ifuatavyo Ethiopia 4-2 Madagascar, Zambia 0-0 Libya, Msumbiji 3-0 Comoros, Sudan 0-2 Ghana, Swaziland 0-1 Congo, Uganda 0-0 Kenya na Guinea-Bissau 0-2 Angola.

Comments