WAWILI WANASWA KWA WIZI WA TIKETI ZA MECHI YA YANGA V AZAM FC

Mmoja wa wauzaji tiketi kwenye mechi ya Azam na Yanga iliyochezwa Septemba 18 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Seleman Masoud aliripoti kupotelewa kitabu kimoja cha tiketi mara baada ya ugawaji wa vitabu hivyo kwa wauzaji kufanyika asubuhi ya siku ya mchezo kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Tiketi kutoka kwenye kitabu hicho ziliuzwa kwa mashabiki ambao walikamatwa. Walitakiwa kuonesha mahali ambapo wameuziwa tiketi hizo ambapo walionesha kwa muuzaji mwingine Salum Abdallah. Abdallah pia alikuwa mmoja wa wauzaji tiketi katika mechi hiyo.
Wauzaji wote wawili walikamatwa na TFF na tukio kuripotiwa Kituo cha Polisi Chang’ombe. Tukio hilo lilifunguliwa jalada namba CHA/IR/6257/2011 ambapo watuhumiwa wameshachukuliwa maelezo yao. Kitabu kilichoibwa kilikuwa na tiketi 100 zenye thamani ya sh. 300,000. Thamani ya kila tiketi ni sh. 3,000.

Comments