WASOMI WATAKIWA KUFANYA TAFITI KWENYE SANAA

Profesa Elias Jengo (Katikati) akimuonesha Katibu Mtendaji wa BASATA,Bw.Materego (Kulia) moja ya kazi za Sanaa zilizoandaliwa na wanafunzi wa Idara ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 
Mkurugenzi wa Kundi la Parapanda Art,Mgunga Mwamnyenyelwa (Kulia) akiwafafanulia jambo wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee waliofika kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Idara ya Sanaa.

 Wanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Tambaza nao hawakuwa nyuma katika kudondosha burudani ya asili kwenye maadhimisho hayo.
Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ambaye ni Katibu Mtendaji wa BASATA Bw.Materego akiwa kwenye picha ya pamoja na wageni waalikwa.


Na Mwandishi Wetu

Wasomi nchini wametakiwa kujikita kwenye tafiti na kuandaa machapisho kuhusu tasnia ya sanaa nchini kwani kumekuwa na uhaba mkubwa wa vitabu na takwimu katika eneo hilo.
Wito huo umetolewa wiki hii na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bw.Ghonche Materego kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 toka kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyoandaliwa na Idara ya Sanaa ya Chuo Kikuu hicho na kufanyika kwenye viwanja vya idara hiyo.

“Tunahitaji kujenga uwezo wa wanafunzi wetu ili kuwa na wataalamu waliobobea katika utafiti,hasa ukizingatia kuwa tafiti katika tasnia mbalimbali za sanaa hapa nchini bado siyo za kutosha sana” alisema Materego.

Aliongeza kwamba,kukosekana kwa machapisho na utafiti kwenye tasnia hii ni chanzo cha wasanii kukosa taaluma muhimu kwa maendeleo na ubora wa kazi zao lakini pia kukosa urithishwaji wa taaluma hii kwa vizazi vijavyo.

“Tunahitaji kuongeza machapisho yanayotokana na wataalamu wetu na kutoka Idara hii,ili kuwawezesha wasomi na wasanii wetu kupata maarifa yanayotokana na mitazamo na falsafa zetu kama wanataaluma wa Kitanzania na Kiafrika” alisisitiza Materego.

Katika hili aliweka wazi kuwa,kuongeza idadi ya wasomi bila kujikita katika utafiti na kuandaa machapisho ya tasnia hii si maendeleo yanayojitosheleza.

Awali akitoa historia ya Idara hiyo,Mhadhiri wa Sanaa Profesa Elias Jengo alisema kwamba ilianza kwa kutoa taaluma ya Sanaa za Maonyesho mwaka 1966 huku ikiwa na wanafunzi wachache sana kabla baadaye Machi 1975 haijabadilishwa na kuwa Idara ya Sanaa,Muziki na Sanaa za Maonyesho.

Aliongeza kwamba,kwa sasa Idara hiyo ina jumla ya wanafunzi kati ya 50-70 huku ikiwa na mafanikio mbalimbali ya kujivunia katika tasnia ya Sanaa.

Comments