VIINGILIO KWA MECHI ZA SIMBA, YANGA CHAMAZI VYAONGEZWA

Tiketi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zinazohusisha timu za Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam hazitauzwa uwanjani. Lengo ni kuwaondolea usumbufu mashabiki ambao wanakwenda kwenye mechi hizo na kukuta tiketi zimekwisha, hivyo kuweza kuwa chanzo cha vurugu.

Ili kujiridhisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilifanya uhakiki na kubaini Uwanja wa Azam una uwezo wa kuchukua watazamaji 5,000 tu na si 7,000 kama ilivyoelezwa awali. Hata hivyo lengo la mmiliki wa uwanja huo ni kuongeza viti hadi kufikia 7,500.
Kwa mantiki hiyo tiketi zitakazouzwa kwa mechi za Yanga na Simba kwenye uwanja huo ni 5,000 tu. Vituo vya kuuzia tiketi hizo siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mchezo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Kituo cha Mafuta cha OilCom kilichoko Ubungo na Mbagala Rangitatu.
Viingilio kwa mechi za timu hizo zitakazochezwa Uwanja wa Azam ni sh. 20,000 kwa jukwaa kuu lenye uwezo wa kuchukua watazamaji 400 wakati majukwaa ya kawaida itakuwa sh. 7,000. Ili kuhakikisha idadi ya mashabiki haizidi uwezo wa uwanja hakutakuwa na tiketi za bure (complimentary).
Hivyo kutokana na kuwepo vituo vya kuuzia tiketi katika maeneo yaliyotajwa, mashabiki ambao watakosa tiketi hawana sababu ya kwenda uwanjani. Simba na Yanga zitaanza kuutumia uwanja huo kesho (Septemba 14 mwaka huu) kwa Simba kuwa mwenyeji wa Polisi Dodoma wakati siku inayofuata Yanga itakuwa mgeni wa African Lyon.

Comments