TFF YAJIVUNIA KUONGEZEKA KWA MAPATO

SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF), chini ya Rais wake Leodegar Chilla Tenga, limefanikiwa kuongeza mapato na matumizi yake kutoka sh milioni 922.4 mwaka 2002 hadi bilioni 6.785 kufikia 2008.
Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya Kamati maalumu iliyokuwa imeundwa na TFF kwa lengo la kudhibiti na kuboresha mapato ya shirikisho hilo, ikijikita zaidi kwenye mapato ya milangoni, udhamini na mengineyo.
Tenga alisema, ongezeko hilo ni la asilimia 663 na ni hatua kubwa kimaendeleo kwa shirikisho hilo na kuongeza kuwa, bado wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi kwa maendeleo ya mchezo huo.
Kwa upande wa timu za taifa, Tenga alisema, uchambuzi wa ripoti hiyo umeonesha mahitaji ya timu zote za taifa kwa mwaka na uendeshaji wa TFF pasipo kujumuisha shughuli nyingine za maendeleo, ni sh bilioni 18.994 kwa mwaka.
Alisema, licha ya shirikisho kutumia kiasi hicho cha fedha kugharamia timu za taifa kwa mwaka, mapato halisi ya shirikisho hilo kwa mwaka ni sh bil 6.785.
Kuhusu changamoto, Tenga alisema ni kusaka mfumo bora wa kudhibiti mapato pamoja na kuongeza kasi ya udhibiti wa mapato ya milangoni kwa kutumia mfumo wa kielektroniki badala ya tiketi za sasa.
Alisema, kinyume cha dhana iliyojengeka kwenye fikra za wengi, kuwa Shirikisho hilo limekuwa likipta fedha nyingi kupitia viingilio vya milangoni, ripoti hiyo imebaini kuwa, mapato ya milangoni ni asilimia 29.9 tu ya mapato yote hadi kufikia 2008.
Kwa mujibu wa hesabu za shirikisho hilo za 2008, asilimia 57.4 ya mapato hayo, yalitokana na udhamini huku viingilio vikiwa ni asilimia 29.9, serikali asilimia 5.4, FIFA asilimia 4.2 na vyanzo vingine vilikuwa asilimia 3.1.
Tenga alisema, changamoto nyingine wanayokabiliana nayo katika mpangilio wa kudhibiti mapato ni mwitikio mdogo wa wadau wa soka viwanjani na wengi kupenda kuingia bure.
Kamati hiyo maalumu ilikuwa chini ya Tenga mwenyewe, Katibu Deogratius Lyato, huku wajumbe ni Makamu wa pili wa Rais wa TFF, Ramadhani Nassib, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu, Idd Kipingu, Kamanda wa Polisi Mstaafu Dl. Mohamed Chicco, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Saalaam, Naibu Kamishna (DCP), Suleiman Kova, Yusuf Nzowa kutoka Ikulu na Victor Swella wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU).

Comments