TFF YAGOMEA MAKUBALIANO YA YANGA, VODACOM

Shirikisho la soka Tanzania (TFF) limegoma kuyatambua maridhiano ya klabu ya Yanga na wadhamini wa kuu wa ligi Kuu ya Bara, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kuhusu jezi za Yanga kutokuwa na doa jekundu.
Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema  kuwa, wanashindwa kutambua makubaliano hayo kwani kanuni za TFF ziko juu ya Yanga, hivyo kimaamuzi Yanga hawako juu ya sheria na kanuni za shirikisho hilo.
“Hata sisi hatuwezi kuwa juu ya kanuni na sheria za Shirikisho la soka Afrika (CAF), hivyo Yanga hawawezi kuwa juu yetu kimaamuzi, kama inawezekana makubaliano hayo yangetushirikisha kama baba wa soka Tanzania,” alisema Wambura.
Wambura alisema wameweka wazi suala hilo ili baadaye timu nyingine zikijitokeza na matakwa ya rangi zake wadhamini wasigome kuwatekelezea matakwa hayo.
Sakata la Yanga kugomea nembo hiyo linatokana na kuwepo kwa doa jekundu ambalo Yanga wameipinga na kudai katiba yao hairuhusu kuvaa kitu chenye rangi nyekundu.

Comments