TAIFA QUEENS YATWAA FEDHA AAG

HATIMAYE Timu ya Taifa ya Netiboli ‘Taifa Queens’ imekuwa ya kwanza kuitoa kimasomaso Tanzania katika mashindano ya All Africa Games yanayoendelea jijini Maputo Msumbiji baada ya kunyakua medali ya fedha jana.
Taifa Queens inayonolewa na Mary Protas ‘Super Coach au Bibi’ na Restuta Lazaro, jana ilijitwalia medali hiyo baada ya kuilaza Botswana kwa magoli 43-35 katika mchezo uliorindima kwenye Uwanja wa I.F.P Munhuana Maputo, Msumbiji.
Hadi kutwaa medali hiyo, Queens iliifunga Kenya 36-35, kabla ya kuikandamiza Ghana 97-24, kisha ikapoteza kwa Zambia 42-46, ikailaza Zimbabwe 46-37 na Msumbiji 92-8.
Ilipoteza kwa Uganda ambao wameibuka wa kwanza na kutwaa dhahabu, 41-52 ikaibuka na kuichapa Afrika Kusini 32-29, kabla ya jana kujihakikishia medali ya fedha kwa kuitambia Botswana 43-37.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Netiboli Tanzania (CHANETA), Rose Mkisi, alisema wameupokea kwa furaha ushindi huo, ambao umewatoa kimasomaso Watanzania kutokana na timu nyingine hadi sasa kutofanya vema katika michano hiyo.
Timu za soka ya wanawake, ‘Twiga Stars’, ngumi za ridhaa na mashua tayari zimeaga huku riadha, judo na paralimpiki ikisubiriwa.

Comments